KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, March 7, 2014

SIMBA, YANGA, COASTAL UNION ZATOZWA FAINI


BODI ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara imezitoza faini faini klabu za Simba, Yanga na Coastal Union kwa makosa mbalimbali ya utovu wa nidhamu wakati wa mechi za michuano ya ligi kuu.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Simba imetozwa faini ya jumla ya sh. milioni 1.5 kwa makosa matatu.

Aliyataja makosa hayo kuwa ni timu hiyo kujihusisha na vitendo vya ushirikina wakati ilipocheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na kocha wake msaidizi, Selemani Matola kumzonga mwamuzi wakati wa mechi dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Alilitaja kosa lingine kuwa ni mshambuliaji Hamisi Tambwe kuonyesha ishara ya matusi wakati Simba ilipocheza na Ruvu Shooting na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2. Kwa mujibu wa Wambura, kila kosa limetozwa faini ya sh. 500,000.

Wambura alisema Yanga na Coastal Union nazo zimetozwa faini ya sh.500,000 kila moja kutokana na mashabiki wake kujihusisha na vitendo vya vurugu wakati zilipomenyana kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Klabu zingine zilizotozwa faini ni Mbeya City kutokana na mashabiki wake kuingia uwanjani ilipomenyana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Klabu hiyo imetozwa faini ya sh. 300,000.

Wambura alisema Bodi ya Ligi imeamua kutoa adhabu hizo baada ya kukutana na kupitia ripoti mbalimbali za mechi za ligi hiyo zilizochezwa hivi karibuni.

Wakati huo huo, Bodi ya Ligi Kuu, imewataka wamiliki wa Uwanja wa Mkwakwani wa mjini Tanga, kufanya ukarabati katika vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji.

No comments:

Post a Comment