'
Monday, March 17, 2014
MDOMO NUSURA UMPONZE RAGE, AWAITA WANACHAMA MBUMBUMBU
HATIMAYE klabu ya Simba jana ilifanya mkutano wa marekebisho ya katiba kwenye ukumbi wa bwalo la maofisa wa polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.
Hata hivyo, mkutano huo nusura uvunjike baada ya Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, kuwaita wanachama wa klabu hiyo mbumbumbu.
Rage alichafua hali ya hewa na kutaka kuzuka tafrani akidai kuwa, wanachama wa klabu hiyo hawana fedha.
"Nataka kila mmoja atambue kuwa, mimi ni Mwenyekiti wa Simba, ndiye naongoza mkutano huu, nyingi mbumbumbu msiokuwa na fedha mnapaswa kutulia,"alisema Rage.
Kauli yake hiyo iliwachefua wanachama hao, ambao walianza kurusha makombora ya maneno makali dhidi yake kabla ya kuwaomba radhi.
Baada ya Rage kuomba msamaha, mkutano uliendelea ambapo wanachama walijadili marekebisho ya katiba na kuyapitisha.
Baadhi ya vifungu vilivyofanyiwa marekebisho ni kupitishwa kwa suala la tawi kutokuwa na wanachama zaidi ya 25- au wasiopungua 50.
Pia wanachama walipitisha pendekezo la kutaka mkutano mkuu wa kawaida ufanyike mara mbili kwa mwaka badala ya mara moja kama ilivyokuwa awali.
Wanachama hao pia walipitisha ibara ya 26 fasili ya tano ya katiba, inayotamka kuwa, mgombea uongozi asiwe aliyewahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment