KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 24, 2017

SIMBA SIMBA SIMBA


NGEBE, tambo na majivuno baina ya mashabiki wa klabu za Yanga na Simba zimemalizika. Jana ilikuwa hukumu kwa timu hizo kongwe katika mchezo wa Ngao ya Jamii.

Timu ya Simba ilitwaa Ngao ya Jamii, baada ya kushinda mabao 5-4 kwa penalti.

Mchezo huo wa kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ulichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mikwaju ya penalti ilitumika ili kupata bingwa, baada ya miamba hiyo ya kandanda kumaliza ndani ya dakika 90.

Penalti za Yanga zilifungwa na Papy Tshishimbi, Thabani Kamusoko, Ibrahim Ajibu, Donald Ngoma wakati Kelvin Yondani, Juma Mahadhi walikosa.

Simba ilipata penalti zake kupitia kwa Method Mwanjali, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Shiza Kichuya na Mohammed Ibrahim 'Mo' wakati Mohammed Hussein 'Tshabalala' walikosa.


Mchezo huo ulikuwa ni moja ya ‘derby’ maarufu Afrika ikishika nafasi ya tatu baada ya Al Ahly vs Zamalek za Misri inayotajwa namba moja.

Nyingine ni ‘Soweto Derby’ baina ya Orlando Pirates vs Keizer Chiefs za Afrika Kusini ikifuatiwa na Simba dhidi ya Yanga.

Awali, mpira ulianza kwa kasi hasa ukichezwa zaidi katikati kwa takribani dakika 10 huku wachezaji wa kimataifa Haruna Niyonzima wa Simba na Papy Tshishimbi, wakionyesha ufundi.

Niyonzima aliyejiunga na Simba kutoka Yanga, alicheza kwa ustadi katika eneo la katikati akisaidiana na Mzamiru Yassin.

Tshishimbi, kiungo wa kimataifa aliyetua Yanga kutoka Mbabane Swallors, aling'ara katika dimba la kati akigawa mipira maridadi kwa washambuliaji wake.

Kiungo huyo raia wa Swaziland mwenye asili ya Jamhuri ya Congo, alicheza pacha na nahodha wake Thabani Kamusoko.

Licha ya kujiunga na Yanga muda mfupi, Tshishimbi, alicheza kwa ustadi kulinganisha na Niyonzima katika mchezo huo.

Simba ilifanya shambulizi la kushitukiza dakika ya 15, lakini Laudit Mavugo, alikosa bao akiwa ndani ya eneo la hatari.

Mavugo, alishindwa kuunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Niyonzima kutoka upande wa kulia mwa uwanja.

Ibrahim Ajibu, mmoja wa washambuliaji hatari nchini, alikosa bao dakika ya 24 kwa kupiga shuti lililotoka pembeni kidogo mwa lango la Simba.

Ajibu ametua Yanga kutoka Simba na jana alicheza kwa kiwango bora na kuwa tishio kwa safu ya ulinzi ya Simba iliyokuwa chini ya mabeki wa kati nahodha Method Mwanjali na Salim Mbonde.

Yanga ilikosa bao dakika ya 30 baada ya Donald Ngoma, kupiga mpira wa krosi uliotua mikononi kwa kipa Aishi Manula.

Simba ilijibu shambulizi dakika tatu baadaye kwa shuti la kiungo wa pembeni Shiza Kichuya kupiga mkwaju uliozuiwa na beki Vincent Andrew 'Dante'.

Niyonzima alikosa bao dakika ya 40, alipounganisha mpira wa kona uliochongwa na Kichuya lakini alifumua shuti juu.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu huku timu zote zikikosa mabao licha ya kutengeneza nafasi za kufunga.

Laudit Mavugo wa Simba nusura afunge bao baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga, lakini shuti lake lilitoka nje kabla ya Kamusoko kukosa bao dakika ya 53.

Lango la Simba lilikuwa katika hatari ya kufungwa bao, baada ya Yanga kufanya shambulizi lakini mabeki waliokoa.

Juma Liuzio alikosa bao dakika ya 75 baada ya kupiga shuti ambalo mabeki wa Yanga walikaa imara kuokoa.

Pia Ajibu alikosa bao dakika ya 77 kwa shuti lake kupaa kabla ya Tshishimbi kufumua shuti dakika mbili baadaye lililokosa mwelekeo.

Niyonzima aliyepewa kadi ya njano na mwamuzi wa mchezo, Elly Sasi, alionekana mara kwa mara akilalamika uwanjani.

Dakika ya 86 Ajibu alikosa bao baada ya kupiga mpira wa krosi kuokolewa na libero Salim Mbonde.

Yanga: Youthe Rostand, Juma Abdul/Hassani Kessy, Gadiel Michael, Vincent Andrew, Kelvin Yondani, Papy Tshishimbi, Thabani Kamusoko, Raphael Daudi/Juma Mahadhi, Donald Ngoma, Ibrahim Ajibu na Emmanuel Martin.

Simba: Aishi Manula, Ali Shomari, Erasto Nyoni/Mohammed Hussein, Method Mwanjali, Salim Mbonde, James Kotei, Mzamiru Yassin/Mohammed Ibrahim, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, Laudit Mavugo/Juma Liuzio na Shiza Kichuya.

No comments:

Post a Comment