KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 9, 2017

'SIMBA DAY' HAIJAPATA KUTOKEA, NIYONZIMA NA OKWI WALITEKA JIJI



SIMBA jana ilisherehekea vyema siku yake baada ya kuichapa Rayon Sports ya Rwanda bao 1-0 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo iliyohudhuriwa na maelfu ya mashabiki, wengi wakiwa wa Simba, ilitawaliwa na matukio mengi, likiwemo utambulisho wa wachezaji wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu huu wa ligi.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, ndiye aliyepewa jukumu la kuwatambulisha wachezaji hao mmoja baada ya mwingine, huku mashabiki wakilipuka mayowe ya kuwashangilia.

Kiungo wa zamani wa Yanga, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi na kipa wa zamani wa Azam, Aishi Manula, ndio walioongoza kwa kushangiliwa kwa mayowe mengi ya mashabiki hao.

Mbali na tukio hilo, mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Mohamed Dewji alipewa heshima ya kuzindua App ya klabu hiyo, ambayo itakuwa na habari zinazoihusu klabu hiyo.

Katika kuongeza shamrashamra, klabu hiyo pia ilitoa tuzo maalumu kwa nyota wa zamani wa timu hiyo, Abdalla Kibadeni, ambaye aliweka rekodi ya kutwaa mataji mbalimbali akiwa kocha na mchezaji.

Kabla ya kuanza kwa pambano hilo, timu hizo zilikaguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, January Makamba, aliyeongozana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Mchemba na Dewji.

Katika mechi hiyo, Simba ilionyesha kiwango kizuri katika safu zake zote tatu za ulinzi, kiungo na ushambuliaji, huku ikifanya mashambulizi mazuri na kwa mpangilio maalumu.

Bao pekee na la ushindi la Simba lilifungwa na mshambuliaji Mohamed Ibrahim, baada ya kupokea pasi maridhawa kutoka kwa Okwi.

No comments:

Post a Comment