KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, tayari kimetua nchini Uganda kwa kambi ya siku 10 ya maandalizi ya msimu ujao utakaoanza Agosti 26 mwaka huu.
Kambi hiyo ni maalumu kabisa kwa ajili ya kucheza mechi nne kali za ushindani, dhidi ya KCCA, URA, SC Villa na Vipers, zitakazotumika kuwajenga wachezaji wa timu hiyo kabla ya mikikimikiki ya ligi kuanza.
Msafara wa Azam FC ulioongozwa na Meneja Phillip Alando, unaundwa wachezaji 26 na makipa Mwadini Ally, Razak Abalora, Benedict Haule, Mabeki ni Nahodha Msaidizi Aggrey Morris, David Mwantika, Yakubu Mohammed, Daniel Amoah, Abdallah Kheri, Swaleh Abdallah, Bruce Kangwa, Hamimu Abdul.
Viungo ni Nahodha Himid Mao ‘Ninja’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo ‘Chumvi’, Stephan Kingue, Salmin Hoza, Bryson Raphael, Masoud Abdallah ‘Cabaye’, mawinga Joseph Mahundi, Enock Atta, Idd Kipagwile, Joseph Kimwaga na washambuliaji Yahaya Mohammed, Mbaraka Yusuph, Wazir Junior, Yahya Zayd.
Kikosi hicho kimefikia kwenye Hoteli ya Top Five, iliyopo Ntinda, jijini Kampala, Uganda, ambapo muda si mrefu benchi la ufundi linatarajia kutoa programu kamili hadi mwisho wa ziara hiyo itakayomalizika Agosti 15 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment