Timu ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro baada ya kuondokewa na beki wao kisiki Salum Mbonde aliyejiunga na Simba hatimaye leo wameingia mkataba na beki wa African Lyon Hassan Suleiman Isihaka.
Timu hiyo inayomilikiwa na kiwanda cha Sukari bora nchini Mtibwa Sugar kilichopo Turiani, imefanikiwa kunasa saini ya beki huyo ambaye msimu uliopita aliichezea kwa mkopo African Lyon ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, baada ya African Lyon kuteremka Daraja msimu uliopita, Isihaka akafikia makubaliano maalum ya kuvunja mkataba na Simba ili awe huru na hivyo kufanikiwa kujiunga na Mtibwa Sugar
Ujio wa beki huyo ni pendekezo la benchi la ufundi la Mtibwa Sugar linaloongozwa na Zuberi Katwila.
“Kiukweli usajili huu niliusubilia kwa hamu yote kubwa nadhani kila kocha anatamani kuwa na mchezaji huyu nadhani bahati imedondokea kwa Mtibwa Sugar , pia natoa shukrani za dhati kwa viongozi kwa kufanikisha usajili huu maana ulikua wa muhimu sana kwangu,” amesema Katwila.
Kwa upande wake. Isihaka amesema kwamba alikua anatamani kufanya kazi na ‘Wana Tam Tam’ kwa muda mrefu; “Nilikua natamani kufanya kazi na Mtibwa Sugar kwa muda mrefu na ninadhani nimefanikiwa kwa kuwa ni klabu kubwa na wachezaji wengi nchini wakubwa wamepita hapa,” amesem Isihaka.
Isihaka anakuwa mchezaji mpya wa saba kusajiliwa na Mtibwa Sugar dirisha hili, wengine wakiwa ni kipa Shaaban Hassan Kado, mabeki Salum Kanoni kutoka Mwadui, Hussein Idd Hante kutoka JKT Oljoro, viungo Hassan Dilunga kutoka JKT Ruvu na washambuliaji ni Riffat Khamis Msuya kutoka Ndanda FC na Salum Ramadhani Kihimbwa ‘Chuji’.
No comments:
Post a Comment