KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, August 14, 2017

KILOMONI AVULIWA UDHAMINI SIMBA, BILIONI 1.3 ZATUMIKA KUSAJILI WACHEZAJI



MKUTANO Mkuu wa klabu ya Simba, umetangaza kumvua wadhifa wa mjumbe wa baraza la wadhamini, mwanachama mkongwe, Hamisi Kilomoni.

Uamuzi wa kumvua nafasi hiyo Kilomoni, ulifikiwa katika mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika jana, kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdalla, alipendekeza mbele ya wanachama 927, waliohudhuria mkutano huo, Kilomoni aondolewe katika Baraza la Wadhamini kutokana na kitendo chake cha kufungua kesi mahakamani kupinga mkutano huo.

Kwa mujibu wa Salim, kwa kufanya hivyo, Kilomoni alivunja Katiba ya Simba
Ibara ya 18 kifungu cha 15 (b), ambayo hairuhusu masuala ya klabu hiyo
kufikishwa mahakamani.

Kilomini ametakiwa kuandika barua ya utetezi na kufuta kesi aliyofungua Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kinyume chake atafutwa kabisa uanachama.

Aidha, mkutano huo ulimpitisha Waziri wa zamani wa Michezo, Profesa Juma Kapuya, kuziba pengo la Ally Sykes katika Baraza la Wadhamini, huku Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaj Adam Mgoyi, akiteuliwa kuziba nafasi ya Kilomoni.    


Katika hatua nyingine, klabu ya Simba imetumia sh. bilioni 1.3, kwa ajili ya usajili wa kikosi cha Simba msimu huu.

Hayo yalisemwa na Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah, katika mkutano uliofanyika jana.

Abdallah alisema wamesajili kikosi madhubuti kwa gharama kubwa, lengo likiwa ni kurejesha heshima ya klabu yao na kwamba, wachezaji wa kigeni pekee wamegharimu sh. milioni 679, zikiwemo sh. milioni 226, zilizotumika katika dirisha dogo, Desemba, mwaka jana.

No comments:

Post a Comment