'
Sunday, August 6, 2017
MR. NICE: SINA NINACHOKIJUTIA KATIKA MAISHA YANGU
HUWEZI kuamini, lakini ndivyo ilivyotokea. Ni kama vile anajutia maisha aliyopitia au kuna mipango inayofanywa na baadhi ya wasanii wenzake kwa lengo la kumwinua tena kimuziki, baada ya kuporomoka kwa kasi ya ajabu na kupoteza umaarufu na utajiri aliokuwa nao miaka kadhaa ya nyuma.
Huyo si mwingine bali ni mkali wa zamani wa miondoko ya Takeu, Lucas Mkenda, maarufu kwa jina la Mr. Nice, ambaye nyota yake ni kama imewashwa upya, kupitia msanii anayetumia lebo ya WCB, Rajabu Abdul 'Harmonize', kwa kumtumia katika somo la kupanda na kushuka kwa maisha ya kila siku ya binadamu.
Harmonize, katika ujio wa wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la ‘Sina’, amemtumia Mr. Nice katika video ya wimbo huo kama muigizaji mkuu wa simulizi ya kisa kinachoelezea kushuka kimaisha na kupoteza marafiki pindi mtu anapoishiwa.
Baadhi ya walioishuhudia video hiyo na kuuona ushirikiano huo, wameanza kuamini kuwa, ni kweli mmiliki wa lebo ya WCB, Abdul Naseeb 'Diamond', amedhamiria kwa dhati kumwinua Mr. Nice, ambaye enzi zake alikuwa hashikiki wala kukamatika.
Kuhusika kwa Mr. Nice katika video hiyo na maudhui ya wimbo huo wa Harmonize, ni dhahiri kwamba hayo ni maandalizi ya ujio mpya wa msanii huyo, ambaye kwa miaka mingi sasa amekuwa akiishi na kufanya shughuli za muziki katika nchi jirani ya Kenya.
Ikumbukwe kuwa, Diamond alishaweka wazi kuhusu uwezekano wa kumsaidia Mr. Nice ili kurejesha makali aliyokuwa nayo miaka kadhaa iliyopita na kumfanya awe na jeuri ya matumizi makubwa ya pesa kila mahali alikokwenda kustarehe.
ENZI ZAKE
Enzi zake, Mr Nice alikuwa hakamatiki. Mtindo wake wa muziki alioubuni na kuupa jina la Takeu, ulimfanya awe maarufu katika ukanda wa Afrika Mashariki. Fedha alizozipata zilimfanya awe na kiburi. Matumizi yake yalikuwa hayaelezeki. Alikuwa msanii jeuri.
Muziki wake ulikuwa ukiuza sio mchezo. Maonyesho yake yalikuwa hayana mfano. Katika baadhi ya nchi alizotembelea, alipokewa kama mfalme huku vijana wakiandamana barabarani kumsindikiza.
Kuna wakati alipokwenda Burundi, alipokelewa uwanja wa ndege wa Bujumbura na waziri mmoja wa nchi hiyo huku akitandikiwa zuria jekundu na msafara wake ukisindikizwa na magari ya polisi. Ni msanii pekee wa Tanzania aliyewahi kupata heshima hiyo.
Mr Nice pia alibahatika kutembelea nchi nyingi za Ulaya kwa ajili ya kufanya maonyesho ya muziki. Marekani, Uingereza, Ujerumani, Sweden, Uholanzi, Dubai, Afrika Kusini kote huko alikuwa akijulikana.
Waswahili wanasema fedha fedheha na pia ivumayo haidumu. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Mr Nice. Haikuchukua muda mrefu umaarufu wake kimuziki na utajiri wake vikatoweka ghafla. Hadi leo hajui nini kilichotokea, lakini anaamini hiyo ni mipango ya Mungu, hakuna mkono wa mtu.
Mr Nice aliwahi kukiri kwamba, alikuwa na fedha lukuki, zote zikiwa kwenye akaunti mbalimbali hapa nchini, lakini zote zilitoweka ghafla bila yeye kujua zimetumikaje. Kila anapoyakumbuka yote hayo, machozi huwa yakimtoka.
Ni kutokana na kuporomoka kwake kimuziki na pengine kukimbia aibu iliyoanza kumpata, Mr Nice akaamua kuhamisha makazi yake kutoka Tanzania kwenda Kenya, akiamini kuwa huenda huko mambo yangemnyookea na angeweza kurejesha hadhi yake kimuziki. Lakini sivyo ilivyokuwa.
MIKASA
Alijikuta akikumbwa na masaibu mengi zaidi. Kuna wakati aliwahi kupata ajali ya gari, wenzake wote aliokuwa nao kwenye gari walilokuwa wakisafiria, walifariki, isipokuwa yeye pekee. Ama kweli kama siku yako haijafika, huwezi kufa.
Pia, aliwahi kuzushiwa kifo mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuvumishwa kwamba alikuwa na ukimwi, baada ya kulazwa kwenye hospitali moja ya mjini Nairobi kwa zaidi ya mwezi mmoja. Alipoibuka na kueleza ukweli kuhusu afya yake, watu wakabaki vinywa wazi. Hadi leo anadunda akiwa na afya njema kabisa.
Mr. Nice pia aliwahi kupigwa mara kadhaa kwenye kumbi za burudani, kama ilivyokuwa enzi zile alipokuwa na ugomvi usiokwisha kati yake na msanii Dudu Baya. Kuna wakati iliwahi kubainika kuwa, waliompiga walikuwa wakitaka kuharibu sura yake, kisa kikiwa ni kuhusishwa na mke wa mtu.
Alipochoka sana kimaisha, ikavumishwa kwamba, aliamua kuwa dereva wa bodaboda. Pia ilikuwa ikidaiwa alikuwa akilala na kukesha kwenye baa kwa vile hakuwa na sehemu ya kulala.
Hiyo ndiyo historia fupi ya maisha na mikasa iliyowahi kumkuta msanii huyu, ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Kilimanjaro, aliyezaliwa na kukulia maeneo ya Kinondoni, Dar es Salaam.
HANA ANACHOJUTIA
Licha ya kukutwa na mikasa yote hiyo kimaisha, Mr. Nice anasema hakuna chochote anachokijutia. Anasema kwake kitu majuto hakipo kwa sababu hakuna kitu chochote ambacho hajawahi kukifanya.
"Hata unifanye nini, mimi ni huyu huyu, hakuna kitu kitakachobadilika. Hakuna ninachoweza kujutia," amesema Mr. Nice, alipohojiwa na kituo kimoja cha televisheni hivi karibuni.
Msanii huyo alisema hawezi kueleza bayana ni kiasi gani cha fedha alichowahi kumiliki wakati alipokuwa maarufu kimuziki kwa sababu hiyo ni siri ya maisha yake, hawezi kuitoa mahali popote wala kwa mtu yeyote.
"Hiyo ni siri yangu. Hakuna aliye na ushahidi ni kiasi gani cha fedha nilikuwa nacho,"amesema Mr. Nice.
Aliongeza kuwa, kuweka fedha kwenye buti la gari kama alivyokuwa akifanya wakati akiwa na hali nzuri kimaisha ni jambo la kawaida, lakini akasisitiza kuwa siyo kila anayefanya hivyo, fedha hizo ni zake, wengine hutafuta ujiko.
Mr. Nice anasema watu wengi wanaamini kuwa, alitumia vibaya fedha alizokuwa akizipata, lakini amesisitiza kuwa, 'hajachoka' kama wengine wanavyofikiria.
"Bado ninazo fedha zilezile. Watu hawajui vitu ninavyovimiliki. Pesa niliyonayo ni ileile niliyokuwa nayo wakati ule kwa sababu kuna vitu niliwekeza, lakini watu hawajui,"alisema na kuongeza:
"Ninayo makoloni mengi. Nikishindwa hapa, nafanya kitu kingine. Msanii unapaswa kuwekeza katika mambo mengine, badala ya kutegemea muziki peke yake. Wapo wasanii wamewekeza kwenye vioski na biashara mbalimbali."
Mr Nice anasema msanii anapokuwa juu, anapaswa kutambua kuwa kuna siku ataporomoka, hivyo ni lazima ajiandae kwa hali hiyo.
WITO KWA WASANII
"Wasanii wengi wakishaporomoka, wanachanganyikiwa. Wengine hukimbilia kutumia dawa za kulevya na kujiharibu kabisa. Wanapaswa kujua kuwa, kama kuna kupanda, pia kuna kushuka," amesisitiza.
Ametoa mwito kwa wasanii nchini wasife moyo kwa sababu muziki una kupanda na kushuka na kwamba, pale msanii anapojiona kuwa yuko juu, ajue pia kuwa wakati wowote mambo yanaweza kuharibika akashuka chini. Anasema hali hiyo iko kwa wasanii kote duniani.
Aidha, amewataka wasanii kuwa na upendo na kuacha majungu na unafiki. Amesisitiza kuwa, kile kidogo wanachokipata kutokana na muziki, wanapaswa kuwekeza kwa sababu kuna leo na kesho.
Mr Nice anasema kwa sasa bado yuko katika Jiji la Nairobi nchini Kenya, ambako ndiko ameamua kuendesha maisha yake, isipokuwa amekuja Dar es Salaam, kwa ajili ya kazi maalumu, ambayo hakuwa tayari kuitaja.
"Bado nipo Nairobi naendelea na mambo yangu. Ukijipanga na usipojali, hata kama mambo yamekwenda mrama, unasema mimi ni mimi. Naendelea na muziki na nitakuwa mwanamuziki hadi siku nitakapokufa,"anasema msanii huyo.
Mr. Nice amesema kwa kuwa muziki ni biashara, anaangalia wapi upepo unakokwenda vizuri na hiyo ndiyo sababu iliyomfanya ahamishie makazi yake mjini Nairobi.
"Wengi anajiuliza kwa nini Mr. Nice amehama nchini na kwenda kuishi Kenya. Ninachopenda kuwaambia ni kwamba, upepo wangu upo kule,"amesema.
Hata hivyo, amesema kuna mipango anayoifanya kwa kushirikiana na baadhi ya watu maarufu nchini, lakini amesisitiza kuwa ni mapema kuitaja.
Lakini baadhi ya wadadisi wanaamini kuwa, ujio wake na kushirikishwa kwake kwenye kibao cha Harmonize, ni utekelezaji wa ahadi ya Diamond, kumrejesha tena msanii huyo kwenye chati ya juu kimuziki.
NYIMBO MPYA
Mr. Nice anasema anazo nyimbo nyingi mpya, ambazo ameshamaliza kuzirekodi, lakini bado hajazisambaza kwenye vituo vya redio na televisheni.
"Ninashirikiana na watu fulani, sitaki kuwataja. Tutafanya mambo makubwa, mashabiki wangu wanivumilie, mambo mazuri yanakuja,"amesema Mr. Nice.
FAMILIA
Msanii huyo ana watoto wawili, wa kike na kiume, lakini hapendi maisha yake ya kimuziki yafanane na yale ya kawaida, ndio sababu hapendi kumpangia mtoto wake yeyote kufuata nyayo zake.
"Siwezi kujua kama wanapenda muziki au la, lakini siwezi kuwalazimisha au kuwatembeza kwenye vyombo vya habari ili wajulikane. Sipendi wawe na maisha yanayofanana na ya kwangu,"amesema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment