'
Sunday, August 20, 2017
WACHEZAJI SIMBA, YANGA KUPIMWA MKOJO
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema wachezaji wa klabu za Simba na Yanga, watafanyiwa vipimo vya mkojo kabla ya mechi yao ya kuwania Ngao ya Jamii, itakayopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Saaam.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema mjini Dar es Salaam, jana, kuwa upimaji huo umelenga kubaini iwapo kuna baadhi ya wachezaji wa timu hizo wanatumia dawa za kuongeza nguvu.
Alfred alisema upimaji wa aina hiyo ni wa kawaida kwa timu zote zinazoshiriki katika michuano ya ligi kuu na hufanyika wakati wowote.
Alisema kitakachofanyika ni madaktari kuchukua vipimo vya mchezaji yeyote watakayemuhitaji kutoka katika kila timu na utasimamiwa na TFF.
"Tumekuwa tukifanya hivi kila mwaka, kabla ya ligi kuanza na zoezi hili hufanywa na madaktari maalumu chini ya usimamizi wa TFF. Huu ni muendelezo wa upimaji huo, haitakuwa mara ya kwanza,"alisema Alfred.
Kwa mujibu wa Alfred, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mechi hiyo yanakwenda vizuri na tiketi zimeshaanza kuuzwa katika vituo mbalimbali ili kuwapa fursa mashabiki kununua mapema, hivyo kujiepusha na usumbufu.
Viingilio katika mchezo huo vimepangwa katika makundi manne. Sehemu ya VIP A tiketi ni sh. 25,000; VIP B na C sh. 20,000; Viti vya rangi ya chungwa sh. 10,000 na mzunguko kwa viti vya rangi za bluu na kijani ni sh. 7,000.
Katika kujiandaa na mechi hiyo, Simba na Yanga zimekwenda Unguja na Pemba kwa ajili ya kuweka kambi, ikiwa ni pamoja na kucheza mechi kadhaa za kujipima nguvu.
Wakati huo huo, habari za kuaminika kutoka ndani ya TFF, zimeeleza kuwa, mwamuzi bora wa ligi kuu msimu uliopita, Elly Sassi, mwenye umri wa miaka 28, ndiye atakayechezesha mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba.
Sassi ndiye aliyeibuka mwamuzi bora wa ligi hiyo msimu uliopita na amekuwa akitabiriwa kufika mbali kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha katika kuchezesha soka.
Mwamuzi huyo kijana pia amekuwa akitajwa kuwa ni mwenye msimamo, anayefuata sheria na kanuni zote za kuchezesha soka, jambo ambalo limemfanya amudu michezo mingi mikubwa, ndani na nje ya nchi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment