Na. Neema Mathias na Thobias Robert- MAELEZO
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewahamasisha Wasanii wa Muziki wa Kizazi kipya nchini kuanzisha mfuko wa wasanii kwa lengo la kutatua changamoto ya udhamini inayowakabili.
Waziri Mwakyembe ametoa wito huo leo Jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na Wasanii hao kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) ambacho kilijadili changamoto mbalimbali zinazowakabili Wasanii na namna ya kukabiliana nazo.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mwakyembe alisema kuwa kutokana na malalamiko na changamoto mbalimbali zinazowakabili Wasanii, ambazo nyingi zinasababishwa na mikataba inayowanyonya Wasanii katika kazi zao, ni vema sasa Wasanii hao kupitia Chama chao cha Tanzania Urban Music Association (TUMA) kuanzisha mfuko ambao utakua unatoa mikopo kwa Wasanii ili kuwezesha utendaji wa kazi zao pasipo kutegemea wadhamini.
“Ninafikiri dawa tunayohitaji ni kuanzishe mfuko wa Wasanii ambapo kila Msanii atatakiwa kuchangia fedha. Jambo ambalo litawavutia wadau wengine kuchangia mfuko huo na kuwaondoa katika dhana ya utumwa, na mfuko huo utamsaidia msanii aliyejisajili kupata mkopo bila kutozwa riba yoyote,” alielezea Waziri Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe alisema kuwa Tasnia ya Sanaa ina mchango mkubwa katika kuongeza pato taifa hivyo ametaka tasnia hiyo kurasimishwa ili kupunguza tatizo la ajira na pia kutumika kama chombo maalumu cha kuielimisha jamii kwani kupitia Sanaa wananchi hupata ujumbe kwa urahisi.
Aidha, Waziri Mwakyembe ameunda Kamati ya kushughulikia masuala yanayowakabili Wasanii ikiwemo sera na sheria ili kuboresha maslahi ya Msanii. Wasanii wanaounda Kamati hiyo ni Azma Mponda, Niki wa Pili pamoja na Witness Mwaijanga.
Katika hatua nyingine Waziri Mwakyembe amelitaka Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kufanyia mabadiliko sera ya Sanaa pamoja na baadhi ya vipengele vya sheria ya Sanaa ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
“Tunahitaji mabadiliko ya sheria ya sanaa haraka. Katika sheria hiyo ni marufuku mmiliki wa vyombo vya habari kulipwa na Msanii ili kupiga wimbo wake, hakuna nchi katika dunia hii ambayo Msanii anatozwa fedha ili wimbo wake upigwe,” alisisitiza.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA Bw. Onesmo Kayanda amesema kuwa, ili kuboresha na kukuza tasnia ya muziki nchini ni lazima kuwepo na soko la uhakika la kazi hizo pamoja na tuzo mbalimbali ambazo zitatumika kutia hamasa kwa wasanii.
Hata hivyo Bw. Kayanda ameongeza kuwa sera, sheria na miongozo ya baraza hilo ihuishwe ili kulinda kazi mbaimbali za Wasanii ikiwa ni pamoja na kuanzisha mfumo wa kielektoniki wa kujisajili ili Serikali iweze kupata mapato halisi kupitia biashara ya muziki.
Kikao hicho ni cha kwanza kufanyika tangu Waziri Mwakyembe ateuliwe katika Wizara hiyo ambapo ameeleza kuwa kikao kazi kitakuwa kikifanyika mara kwa mara na atakuwa akikutana na wasanii wa vikundi mbalimbali ili kujadili mambo yanayohusu Wasanii hao.
No comments:
Post a Comment