'
Thursday, October 13, 2011
SERIKALI Z'BAR YANAWA MIKONO KWA ZFA
SERIKALI ya Zanzibar imesema haina uwezo wa kuwaondoa madarakani viongozi wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA).
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Zanzibar, Abdilah Hassan Jihadi alipokuwa akijibu maswali ya viongozi wa klabu za soka za Zanzibar.
Kikao kati ya waziri huyo na viongozi hao wa klabu, kilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye hoteli ya Bwawani mjini hapa.
Jihadi alisema serikali haiwezi kuingilia masuala ya ndani ya chama hicho kwa sababu kufanya hivyo ni kwenda kinyume na kanuni za Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).
Alisema iwapo wadau wa soka wa Zanzibar wanauona uongozi uliopo sasa ZFA haufai, wanachopaswa kukifanya ni kufuata katiba ya chama hicho.
“Lakini kwa sasa haitawezekana kwa serikali kuingilia mizozo yoyote ndani ya chama hicho kwa sababu kanuni za FIFA haziruhusu serikali kuingilia kati masuala ya soka,”alisema.
Waziri Jihadi pia aliwatahadharisha wadau wa soka visiwani humo kuacha kukimbilia mahakamani kudai haki kwa sababu kufanya hivyo ni kwenda kinyume na kanuni za shirikisho hilo.
Amewataka wadau hao kuacha kuilaumu ZFA moja kwa moja kwa kutokana na kukabiliwa na migogoro ya mara kwa mara kwa sababu baadhi inasababishwa na wanachama wake.
Alisema matatizo ya uongozi ndani ya chama hicho yamechangiwa na wanamichezo wenye sifa kushindwa kujitokeza kuwania uongozi wakati wa uchaguzi.
Waziri Jiohadi alisema badala yake, wanamichezo hao wamekuwa wakiwaacha watu walewale kuwania uongozi wa chama hicho kila mara na matokeo yake wanashindwa kuleta mabadiliko.
"Suluhisho la kuwandoa viongozi hawa madarakani ni kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi wakati wa uchaguzi badala ya kuwaachia watu wale wale. Mkifanya hivyo, inamaanisha kwamba nyingi wenyewe hampo tayari kwa mabadiliko,”alisema.
Awali, Katibu wa klabu ya Miembeni, Mbarouk Ali aliitaka serikali kutafuta mbinu za kuwatimua madarakani viongozi wa ZFA kwa madai ya kushindwa kuleta mabadiliko.
Mbarouk alidai kuwa, soka ya Zanzibar inazidi kudumaa kwa sababu viongozi wa chama hicho hawapo makini katika kutekeleza majukumu yao.
Kiongozi huyo wa Miembeni alisema, hata kama watapatikana wafadhili, ni vigumu kwa soka ya Zanzibar kupata maendeleo kutokana na viongozi wa ZFA kushindwa kuona mbali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment