KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 13, 2011

TENGA: Fedha za FIFA ni kwa miradi ya maendeleo



SHIRIKISHO la Soka la Dunia (FIFA), halitoi fedha kwa nchi wanachama wake kwa ajili ya kugawana, bali linagharamia miradi ya maendeleo ya soka na mambo mengine yanayohusiana na mchezo huo.
Ufafanuzi huo umetolewa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye hoteli ya Bwawani mjini hapa.
Tenga alitoa ufafanuzi huo baada ya waandishi wa habari kutaka kufahamu matumizi ya dola 250,000 za Marekani zinazotolewa kila mwaka na shirikisho hilo kwa TFF.
“Kwanza si kweli kwamba FIFA huwa ikitoa pesa hizi taslimu kwa nchi wanachama kama baadhi ya watu wanavyofikiria.Fedha hizo ni makisio ya miradi mbalimbali ya kuendeleza soka na miundombinu ya kurahisisha maendeleo ya mchezo huo,”alisema.
Aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na kuinua soka ya wanawake, kuimarisha timu za vijana, kuandaa mafunzo kwa makocha na waamuzi.
"Watu wanazungumza mambo wasiyoyajua. Wanadhani TFF inamwagiwa fedha na FIFA ili tugawane, hii ni dhana potofu,”alisema Tenga.
“FIFA imeainisha maeneo ya kusaidia, lakini sisi tunatakiwa tuandike mapendekezo ya miradi iliyokadiriwa kwa kiasi hicho cha fedha, hatuletewi pesa tutumie," aliongeza.
Akifafanua zaidi, Tenga alisema Zanzibar imekuwa ikinufaika na miradi hiyo kwa vile kila TFF inapoandaa semina za makocha na waamuzi, hukishirikisha chama hicho.
Aliongeza kuwa, tayari viongozi wa vyama hivyo viwili wameshakutana na kukubaliana kuhusu miradi kadhaa, ambayo itazishirikisha pande hizo mbili za muungano kwa manufaa ya soka ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment