'
Thursday, October 13, 2011
CAPELLO AMWEKA ROONEY KITANZINI
LONDON, England
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya England, Fabio Capello amemuonya mshambuliaji Wayne Rooney kuwa, huenda asiichezee timu hiyo katika fainali za Mataifa ya Ulaya za mwaka 2012.
Onyo hilo la Capello limekuja siku chache baada ya Rooney kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi ya hatua za awali dhidi ya Montenegro iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Podgorica, ambapo timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.
Kadi hiyo itamfanya Rooney akose mechi mbili za kwanza za hatua ya makundi katika fainali hizo, zinazotarajiwa kuandaliwa kwa pamoja na Poland na Ukraine.
Capello amesema hata kama Rooney, anayechezea Manchester United atamaliza adhabu hiyo, uwezekano wa kurejeshwa kwenye kikosi hicho ni finyu.
Kocha huyo raia wa Italia amesema pia kuwa, Rooney hatacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Hispania, inayotarajiwa kupigwa mwezi ujao. Alisema nafasi yake itachukuliwa na Danny Welbeck.
Uamuzi wa mwisho kuhusu adhabu ya Rooney unatarajiwa kutolewa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA), inayotarajiwa kukutana mwezi ujao.
Hata hivyo, Capello amesema atamjumuisha Rooney kwenye kikosi chake kitakachocheza fainali hizo hata kama atafungiwa na UEFA kucheza mechi mbili.
“Natumaini atafungiwa mechi moja. Nadhani mwamuzi Wolfgang Stark, atamsaidia Rooney kwa kuieleza UEFA kwamba alikubali adhabu ya kadi nyekundu bila kuonyesha kitendo kingine cha utovu wa nidhamu,” amesema Capello.
Kocha huyo amesema, iwapo atalazimika kumuacha Rooney, hawezi kuwa na wasiwasi wa safu yake ya ushambuliaji kwa sababu anao washambuliaji wa kutosha.
“Katika maisha yangu kama kocha, huwa nakuwa na washambuliaji wengi wazuri. Siku zote huwa nikiamua nani ni bora zaidi kwa wakati huo,”alisema kocha huyo.
Capello alisema anapaswa kuanza sasa kumuandaa mchezaji atakayecheza nafasi ya Rooney katika mechi tano au sita watakazocheza kabla ya fainali za Mataifa ya Ulaya.
Alisema katika baadhi ya mechi hizo, amepanga kumwingiza Rooney kipindi cha pili badala ya kumwanzisha tangu mwanzo.
Kocha huyo alisema ni vigumu kwake kumrekebisha Rooney kwa sababu hawezi kuingia kichwani mwake wakati anacheza.
“Naweza kuzungumza naye kabla, naweza kumtoa uwanjani, naweza kupata suluhisho tofauti. Lakini vitendo vya wachezaji huwezi kuvielewa wanapokuwa mchezoni. Hii si kwa Rooney pekee,”alisema.
“Tukio hilo lilitokea mbele yangu na nilimuona Rooney akimkwatua mchezaji, hivyo nafikiri kadi aliyoonyeshwa ilikuwa sahihi,”aliongeza.
Capello alisema wanapaswa kuanza sasa kukiandaa mapema kikosi cha wachezaji 11 wa England kitakachoanza fainali za Ulaya.
“Rooney hatacheza dhidi ya Hispania. Nataka kuwajaribu wachezaji wapya, staili mpya na mfumo tofauti. Ninao washambuliaji wengi wazuri. Nataka kupata suluhisho lililo bora,”alisema.
Capello alisema anafurahia kuona kuwa, wachezaji wawili, ambao hawamo kwenye kikosi chake, wanacheza vizuri kwa sasa kwenye klabu zao, hivyo kujihakikishia nafasi hiyo. Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Jermain Defoe na Daniel Sturridge.
Kocha huyo pia anatarajia kuwaandaa Darrent Bent na Welbeck kuchukua nafasi ya Rooney. Wachezaji hao wawili walikuwemo kwenye kikosi kilichomenyana na Montenegro.
“Welbeck alicheza kwa dakika 15 dhidi ya Montenegro na alicheza vizuri. Nitamjaribu wakati atakapocheza dhidi ya Hispania.
“Nilitaka kuwaona Bobby Zamora na Andy Carroll. Hawa ni wachezaji, ambao tuko pamoja nao kwa muda kidogo. Zamora ni mchezaji mwenye mvuto na tunahitaji kumuona akicheza dhidi ya timu muhimu,”alisema kocha huyo.
“Nataka kupata suluhisho katika mechi moja ama mbili, ambazo Rooney hatacheza. Na kama tutapata suluhisho, atalazimika (Rooney) kufanyakazi ya ziada kurejea kwenye kikosi cha kwanza. Huo ndio ukweli uliowazi. Ninao wachezaji 23,”aliongeza kocha huyo.
Alipoulizwa iwapo Rooney hataichezea England hadi fainali za za Ulaya zitakapomalizika, Capello alicheka na kusema: “Atakuwa katika hali nzuri.”
Tayari Chama cha Soka cha England kimeshaanza kuchukua hatua za kumlinda Rooney ili kumwepusha na lawama zilizoelezwa kwake. Lengo la chama hicho ni kuona kuwa, Rooney anajifunza kutokana na makosa yake.
Capello pia amepanga kumjaribu beki Phil Jones kucheza na John Terry katika safu ya ulinzi. Alisema Jones alicheza vizuri dhidi ya Montenegro na atakuwa muhimu kwao.
Alimsifu Terry, anayechezea Chelsea kwamba ni nahodha mzuri uwanjani na kwenye vyumba vya wachezaji. Pia alisema ni kiongozi mzuri kwa wenzake.
Akizungumzia nafasi ya kikosi chake kwenye fainali hizo za Ulaya, Capello alisema ana matumaini makubwa ya kufanya vizuri.
Alisema wachezaji wake hucheza vizuri wanapoelekeza akili yao kwenye mchezo, lakini wakati mwingine hupoteza mwelekeo wakati wapinzani wao wanapocheza kwa kasi.
“Kwa sasa tunacheza vizuri na tunaweza kufanya vizuri zaidi. Usisahau baadhi ya wachezaji muhimu ni majeruhi kwa sasa ama hawapo kwenye kiwango kizuri.
“Jack Wilshere ni muhimu. Steven Gerrard ni mchezaji mwingine muhimu. Kwa sasa tunao Gary Cahill na Jones. Kyle Walker pia ni mchezaji mzuri. Vivyo hivyo kwa Micah Richards. Rio Ferdinand anahitaji kucheza mechi nyingi zaidi,”alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment