Nikaona nifike Mwitongo, nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere bila kuliona kaburi lake haiwezekani. Nikaomba ruhusa, nikapiga picha pembeni ya kaburi lake na kumuombea dua. Mola ailaze peponi roho ya Baba wa Taifa. Baadhi yetu watanzania hatutayasahau yale yote uliyotutendea wakati wa utawala wako.
Chakula hiki nilikumbana nacho mara baada ya kufika Butiama. Ni ugali wa muhogo na ulezi, nyama na maharage. Nilikuwa na njaa kwelikweli, japokuwa maharage hayakuwiva vizuri, nilikula hadi nikamaliza.
Hii ndiyo nyumba ya kulala wageni niliyofikia baada ya kufika Butiama. Bei yake ni ubwete tu sh. 3000 kwa usiku mmoja, lakini vyumbani hakuna vyandarua.
Si kwamba magari haya aina ya Noah yapo sokoni, bali usafiri huu ndio unaotumika kwa safari ya kwenda Butiama na Kiabakari. Usafiri huu unaanzia kwenye stendi ya Bweri kwa bei ya sh. 2500 hadi Butiama.
Chakula hiki nilikutana nacho Musoma Mjini. Ni ugali uliochanganywa unga wa muhogo na mtama. Mboga ilikuwa sangara aliyekaangwa na mchuzi kidogo. Hongera sana Wakurya na Wajita.
Hiivi ndivyo safari ilivyoanza. Nilitumia usafiri wa basi la Sumry, nikakaa siti ya nyuma kabisa. Mirusho tuliyoipata huko nyuma kila tulipopita kwenye matuta, haisemeki. Tulipiga kelele hadi tukachoka, dereva hakujali. Nikaona bora tu kufika salama. Kila dereva alipopunguza mwendo, abiria tuliinuka vitini kujiandaa kwa mirusho. Wakati mwingine alipita kwenye matuta bila kupunguza mwendo.
Kama nilivyoeleza wiki iliyopita, kwa muda wa takriban wiki moja nilikuwa safarini katika kijiji cha Butiama wilayani Musoma Vijijini mkoani Mara kwa ajili ya kuandika makala za kumbukumbu ya miaka 12 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Safari hiyo ilinifikisha Mwanza, Musoma Mjini hadi Butiama. Kwa kuanzia, ninawaletea picha za matukio mbalimbali wakati wa safari hiyo.
No comments:
Post a Comment