'
Thursday, October 13, 2011
BECKHAM: Narudi Man Utd
LONDON, England
KIUNGO nyota wa zamani wa England, David Beckham amedokeza kuwa, anataka kurejea kwenye klabu yake ya zamani ya Manchester United.
Hata hivyo, Beckham, ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Los Angeles Galaxy ya Marekani amesema, anataka kurudi Man Utd akiwa mkurugenzi wa michezo.
Beckham (36) alianza kucheza soka Manchester United akiwa na umri wa miaka 14, ambapo aliichezea kwa miaka 10 kabla ya kujiunga na Real Madrid ya Hispania mwaka 2003.
Licha ya msimamo wake huo, klabu za Tottenham, Queen Park Rangers za Uingereza na Paris St Germain zimeonyesha nia ya kumsajili kiungo huyo.
Klabu hizo tatu zinamwania Beckham, kufuatia mkataba wake na Galaxy kukaribia kumalizika.
Beckham aliichezea Manchester United mechi 399 na kushinda mataji ya ligi kuu, Kombe la FA na ubingwa wa Ulaya mwaka 1999.
“Ndoto yangu ni kurudi Manchester United. Ningependa kuwa kama Zinedine Zidane,”alisema Beckham.
Zidane, ambaye alicheza pamoja na Beckham kwenye kikosi cha Real Madrid, kwa sasa ndiye mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo yenye makao yake makuu uwanja wa Bernabeu.
“Ningependa nifanye hivyo. Kumbukumbu yangu nzuri ilikuwa mwaka 1999 wakati Manchester United iliposhinda mataji matatu, hilo halina wasiwasi,”alisema.
“Kwa maoni yangu, hakuna klabu inayoweza kurudia rekodi hiyo,”aliongeza.
Wakati Beckham alipoondoka Old Trafford na kwenda Hispania miaka minane iliyopita, alisisitiza kuwa, asingependa kucheza tena katika klabu nyingine ya ligi kuu ya England zaidi ya Manchester United.
Katika majira ya barido mwaka jana, Beckham alitumia mapumziko ya ligi nchini Marekani kufanya mazoezi na kikosi cha Tottenham, kinachonolewa na Kocha Harry Redknapp.
Redknapp alikiri hivi karibuni kuwa, angependa kumwalika tena Brckham, lakini anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa PSG na QPR, ambazo zote zimeonyesha nia ya kumtaka mkongwe huyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment