SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeusogeza mbele kwa siku moja mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Yanga na Kagera Sugar.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, pambano hilo lililokuwa lichezwe leo, sasa litachezwa kesho.
Wambura alisema wameamua kusogeza mbele pambano hilo, kufuatia maombi ya uongozi wa Yanga.
Alisema katika maombi yao, Yanga ilitaka mechi hiyo ichezwe Ijumaa, siku ambayo ni ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere.
“Kimsingi, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imelikubali ombi hilo la Yanga na mechi hiyo sasa itachezwa Ijumaa,”alisema.
Kwa mujibu wa Wambura, tayari TFF imeshawasiliana na viongozi wa Kagera Sugar na kuwafahamisha kuhusu mabadiliko hayo.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Villa Squad umepanga kutoa tamko la kuwasimamisha baadhi ya wachezaji wake kesho.
Uamuzi huo wa Villa umekuja baada ya Villa kunyukwa mabao 6-0 na Coastal Union katika mechi ya ligi kuu ya Bara, iliyochezwa wiki iliyopita.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka Villa zilieleza kuwa, uongozi umepanga kuwahoji wachezaji kabla ya kutoa uamuzi dhidi yao.
No comments:
Post a Comment