KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 13, 2011

ZFA hatarini kutimuliwa Bwawani


UONGOZI wa hoteli ya Bwawani umekitaka Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kulipa deni la kodi ya ofisi iliyopanga, vinginevyo kijiandae kutimuliwa.
Ofisa Mipango wa hoteli hiyo, Omar Said Ameir alilieleza gazeti la Burudani juzi mjini hapa kuwa, chama hicho kinadaiwa sh. milioni 7.4.
Kwa mujibu wa Omar, fedha hizo ni malimbikizo ya kodi ya pango kuanzia Aprili mwaka jana hadi Septemba mwaka huu.
Alisema uongozi wa hoteli umeshakiandikia barua chama hicho, kukikumbusha wajibu wake wa kulipa deni hilo kama walivyokubaliana wakati wa kupangishwa na kusisitiza kuwa, hautasita kukitimua ofisini.
Omar alisema lengo la uongozi wa hoteli ni kuhakikisha wapangaji wote wanalipa madeni yao kwa wakati mwafaka ili iweze kujiendesha kwa ufanisi.
Uchunguzi wa Burudani umebaini kuwa, uamuzi wa hoteli hiyo kufuatilia madeni hayo, umetokana na agizo la Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Mifugo, Uwezeshaji, Habari na Utalii, ambayo katika ziara zake kwa taasisi hizo, ilihimiza kufuatiliwa kwa madeni hayo.
Kamati hiyo pia ilishauri kutowaonea haya wadaiwa sugu, na kuagiza endapo watashindwa kulipa, waondoshwe mara moja.
"Tunazidai taasisi nyingi, ambazo baada ya kuzifuatilia, zimeanza kulipa na nyingine angalau zinakuja kuzungumza namna ya kusawazisha madeni yao, lakini inasikitisha ZFA hailipi wala haiji ili tushauriane njia ya kumaliza deni lao", alisema ofisa mipango huyo.

No comments:

Post a Comment