KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, August 6, 2017

ACHENI KUNIZUSHIA KIFO ILI MUUZE MAGAZETI-MAJUTO



MUIGIZAJI nyota na mkongwe wa filamu nchini, Amri Athumani, maarufu King Majuto, amevitaka vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuacha tabia ya kumzushia kifo kwa lengo la kuuza magazeti.

Amesema amekuwa akichukizwa na tabia hiyo kwa kuwa imekuwa ikiwashtua ndugu, jamaa na marafiki zake kwa kuamini kuwa ni kweli amekufa, hivyo kukusanyika kwa wingi nyumbani kwake kwa lengo la kuhudhuria mazishi.

Majuto, ambaye alianza uigizaji tangu miaka ya 1970, amesema ameshazushiwa kifo zaidi ya mara tano, hivyo kuwataka waandishi na wamiliki wa vyombo vya habari, kuacha kuchapisha taarifa, ambazo hawana uhakika nazo.

"Kusema kweli haipendezi. Kuweni na taarifa za uhakika, sio hujaipata sawa sawa, lakini kwa sababu unataka kuuza gazeti, unaitoa haraka haraka,"amesema Majuto, alipohojiwa na kituo kimoja cha televisheni hivi karibuni.

"Ninao ndugu zangu wengi nje ya nchi, taarifa hizi ziliwashtua. Kuweni wastaarabu,"amesisitiza msanii huyo, ambaye pia ni mahiri kwa filamu za vichekesho.

Majuto amesema taarifa za hivi karibuni kwamba amekufa, zilitokana na mwandishi mmoja wa habari kusambaza picha zake kwenye mitandao, zikumuonyesha alipokuwa amelazwa kwenye hospitali moja mjini Tanga.

"Wiki moja kabla ya kusambazwa kwa picha hizo, kuna gazeti moja liliandika kwamba nipo hoi, naumwa ngiri wakati sikuwa naumwa. Huyu mwandishi aliyeandika habari hizi ni kama vile alikuwa mchawi wangu kwani haikuchukua hata siku 10, wakati natoka Kenya kufanya maonyesho, nikaanza kuumwa,"amesema King Majuto.

"Wakati nipo hospitali, kuna mtu alinipiga picha, akairusha kwenye gazeti. Wakaweka picha yangu nikiwa mzima nimevaa suti, wakaweka nyingine nikiwa nimelazwa na nyingine ya jeneza na kaburi.

"Nilipoichunguza ile picha ya mazishi na jeneza, nikagundua kwamba zilikuwa picha za mazishi ya marehemu Sharo Milionea. Picha hizi zilitapakaa hadi nje ya nchi. Hapa nyumbani palijaa watu kuja kuzika. Nikaona huu sasa ni mkosi,"amesema msanii huyo, ambaye ameigiza zaidi ya filamu 500.

Majuto amesema kuna wakati aliwahi kuzushiwa kifo alipokwenda kuhiji Makka miaka mitatu iliyopita, jambo ambalo halikuwa la kweli.

"Uzushi ulionikera zaidi ni ule nilipokwenda kuhiji Makka. Nilipofika tu Dubai, nikazushiwa nimefia njiani. Nilipofika Makka, ulitokea upepo mkali, nikazushiwa nimekufa. Tulipokuwa tukijiandaa kutoka Makka kwenda Madina, nikazushiwa tena nimekufa. Wakati wa kurusha mawe kwa shetani, Watanzania 50 walipoteza maisha, nikazushiwa nami nilikufa, wakati sio kweli,"amesema msanii huyo.

Akizungumzia afya yake kwa sasa, Majuto amesema anamshukuru Mungu kwamba anaendelea vizuri na anaweza kurejea katika shughuli zake za kawaida baada ya muda si mrefu.

"Kuishi ukiwa mzima ama ukiwa mgonjwa ni mipango ya Mungu. Nabii Ayubu aliishi karne nyingi akiwa mgonjwa hadi akawa anatoka funza mwilini, lakini akaja kupona,"amesisitiza nguli huyo wa filamu nchini.

"Nikiumwa najua ni sunna, lazima niumwe. Na nikifa ni faradhi, lazima nife. Baba yangu na mama yangu hawapo, hata Rais wangu niliyekuwa nikimpenda, Mwalimu Nyerere hayupo, lazima nife," ameongeza.

Majuto amekiri kuwa, sanaa ya filamu na maigizo ya jukwaani imemwezesha kuwa na maisha mazuri, ikiwa ni pamoja na kumiliki magari, mashamba na kuwasomesha watoto wake katika shule za kulipia.

Amesema hakuna mtoto wake aliyesoma shule ya sekondari ya serikali na kwamba, waliofika chuo kikuu wamemaliza, wanaofanyakazi wanafanya na kusisitiza kuwa, hakuna mtoto wake, ambaye hakuna kitu kichwani.

King Majuto anasema awali, alikuwa akimiliki magari zaidi ya saba, lakini sasa ameyapunguza na kubaki matatu baada ya kuona biashara ya daladala haiendi vizuri.

"Niliamua kuachana na biashara ya daladala kwa sababu mara dereva kaleta hesabu, mara hakuna, nikaona nisije nikapata kichaa,"amesema.

Aidha, King Majuto ameanzisha kampuni yake ya kutengeneza filamu, inayojulikana kwa jina la Kings Movied Ltd na kusisitiza kuwa, hana wasiwasi wa ugali wa watoto kwa kuwa fedha alizonazo, zitaiwezesha familia yake kuishi vizuri hadi atakapoitwa na Mungu.

Akizungumzia maendeleo ya fani ya filamu nchini, amesema wapo wasanii wengi wazuri chipukizi na wenye vipaji vya fani hiyo, lakini hawajiamini. Amewataka kuacha woga na kujituma kwa bidii.

Kabla ya kuwa mwigizaji, King Majuto alikuwa mwajiriwa wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na baadaye kujihusisha na kazi ya ulinzi katika kiwanda cha mablanketi na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) miaka ya 1960.

Alianza kupata umaarufu baada ya kujiunga na kikundi cha DDC Kibisa, ambako ndiko alikobatizwa jina la King Majuto, kutokana na kutunga maigizo mengi yanayotia simanzi.

Baadhi ya filamu alizocheza na kupata umaarufu ni Ndoa ya Utata, Daladala Nimekuchoka,Mbegu, Zebra, Shikamoo Mzee, Tabia, Utani, Tikisa, Trouble Maker, Gundu, Kizungunguzu, Shoe Shine, Street Girl, Faithful, Mtego wa Panya, Boss, Back with Tears, Sikukuu ya wajinga, Nyumba nne, Chips kuku,
Kitu bomba, Ndoto ya tamaa, Lakuchumpa na ATM.

Nyingine ni Bishoo, Tupo wangapi, Moto bati, Varangati, Out side, Pusi na Paku,  Juu kwa Juu, Swagger, Oh Mama, Jazba, Mke wa mtu sumu, Mbugila, Kidumu, Mkali Mo, Mpela Mpela, Utanibeba, Babatan, Mjomba, Msela wa Manzese, Karaha, Mpango sio matumizi, Mume bwege, Shuga Mammy,
Embe Dodo, Nakwenda kwa mwanangu, Seaman, Naja leo naondoka leo.

No comments:

Post a Comment