'
Sunday, March 9, 2014
YANGA YAFAN KIUME, YATOLEWA NA AL AHLY KWA PENALTI
YANGA SC imetolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya jumla ya kufungana bao 1-1 na Al Ahly katika mechi mbili za Dar es Salaam na Alexandria.
Yanga SC iliyoshinda 1-0 wiki iliyopita Dar es Salaam, leo imefungwa 1-0 baada ya dakika 90 kwenye mchezo wa marudiano Uwanja wa Border Guard mjini Alexandria.
Kipa Deo Munishi ‘Dida’ alipangua penalti mbili mfululizo ya nne na ya tano, lakini Yanga SC nao wakakosa penalti mbili mfululizo ya nne na ya tano.
Oscar Joshua alipiga penalti nzuri ikaguswa na kipa Sherif Ekramy Ahmed na kugonga mwamba na kurudi uwanjani, wakati Said Bahanuzi akapiga nje upande wa kushoto wa lango.
Sherif Ekramy Ahmed alipangua penalti ya mwisho ya Yanga SC iliyopigwa na Mbuyu Twite na kuwavusha Hatua ya 16 Bora mabingwa hao wa Afrika.
Waliofunga penalti za Yanga SC ni Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Didier Kavumbangu na Emmanuel Okwi.
Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao, Yanga SC wakicheza mchezo wa kujihami na mashambulizi ya kushitukiza.
Mrisho Ngassa alicheza vyema katika safu ya kiungo mchezeshaji akiwapa pasi nzuri washambuliaji Emmanuel Okwi, Simon Msuva, Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza.
Kiungo mkabaji Frank Domayo alishirikiana vizuri na mabeki wa kati Kevin Yondan na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wakati mabeki wa pembeni Mbuyu Twite kulia na Oscar Joshua kushoto walifanya kazi nzuri ya kuzuia na kusaidia mashambulizi
Kipa Deo Munishi ‘Dida’ alifanya kazi nzuri ya kulinda lango na kuwapanga mabeki wake, pia akianzisha haraka mashambulizi kila alipodaka mpira.
Dakika ya 21 mshambuliaji hatari wa Ahly, Amr Gamal alipata pasi nzuri ndani ya 18 akapiga nje kabisa kulia mwa lango.
Dakika ya 23 Abdallah Said alipiga shuti kali akiwa nje ya 18 likatoka nje sentimita chache kushoto mwa lango na Yanga SC iliwashitua kwa mara ya kwanza Ahly dakika ya 29 baada ya winga Simon Msuva kushindwa kuumiliki vyema mpira mrefu akiwa anatazamana na kipa ukamgonga na kutoka nje kulia mwa lango.
Mabeki wa Ahly waliwadhibiti washambuliaji wa Yanga dakika zote 45 za kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili, Yanga SC walikianza vizuri wakiwabana Al Ahly na kudhibiti mashambulizi yao, huku wao wakiendelea kushambulia kwa kushitukiza.
Dakika ya 55 Simon Msuva almanusra aipatie bao Yanga SC baada ya kupiga shuti akiwa ndani ya 18, lakini likatoka nje sentimita chache upande wa kushoto wa lango akiwa upande wa kulia amebanwa na mabeki wawili wa Ahly.
Ahly wakajibu shambulizi hilo haraka na kupata mpira wa dhabu ambao ulipopigwa dakika hiyo hiyo ya 55 ukasababisha kizaazaa langoni mwa Yanga, lakini Cannavaro akaokoa.
Yanga SC ilipata pigo dakika ya 65 baada ya nyota wake, Mrisho Ngassa kuumia na kutolewa nje nafasi yake ikizibwa na Athumani Iddi ‘Chuji’ dakika ya 66.
Ahly ilipata bao lake dakika ya 71, mfungaji Said Abdulwahed.
Baada ya bao, Ahly walikuwa wanashambulia mfululizo, sifa zimuendee kipa Dida aliyeokoa michomo kadhaa na mingine kutoka nje.
Baada ya dakika 90 kumalizika Ahly ikishinda 1-0, mchezo ulihamia kwenye mikwaju ya penalti na ndipo, safari ya Yanga ilipofikia tamati michuano ya Afrika, wakiendeleza utamaduni wao wa kutolewa mapema.
Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Deogratius Munishi 'Dida', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Mrisho Ngassa/Athumani Iddi ‘Chuji’ dk66, Didier Kavumbagu, Hamisi Kiiza/Said Bahanuzi dk85 na Emmanuel Okwi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment