'
Sunday, March 9, 2014
MBEYA CITY YALALAMIKIA UBABE WA RHINO RANGERS
NA SOLOMON MWANSELE,MBEYA.
UONGOZI wa timu ya Mbeya City F.C,umelalamikia mchezo wa kibabe ulionyeshwa na wachezaji wa timu ya Rhino Rangers,katika mechi iliyochezwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, uliochezwa Machi 8,mwaka huu katika uwanja huo, Mbeya City maarufu zaidi City Boys, iliibuka kidedea kwa kuifunga Rhino magoli 3-1.
Ofisa Habari wa Mbeya City,Freddy Jackson, alisema kutokana na mchezo huo wa kibabe ulioonyeshwa na wachezaji wa Rhino,wachezaji wao wawili kuumizwa vibaya na mlinda mlango wa timu hiyo pinzani.
Jackson alisema Richard Peter aliumizwa kjwa makusudi na kipa wa Rhino (hakumtaja jina), kwa kumrukia vibaya kwa miguu yote miwili na kumsababishia madhara kwenye mbavu zake za kushoto.
“Peter yupo kambini na anaendelea kutibiwa chini ya uangalizi wa karibu kutoka kwa madaktari wa hospitali ya Rufani Mbeya kwa kushirikiana na daktari wetu wa timu” alisema Jackson.
Aliongeza pia mchezaji Mwigane Yeya naye aliumizwa na kipa huyo wa Rhino Rangers baada ya kurukiwa vibaya na kukwaruzwa kwa vidole katika macho yake hali iliyopelekea kushindwa kuona kabisa.
Ofisa Habari huyo alisema vile vile Mbeya City F.C hawakufurahishwa na nidhamu iliyoonyeshwa na Kocha msaidizi wa Rhino Rangers, ambaye alidai muda wa mchezo alikuwa akitoa maneno yasiyo na staha, tofauti na mchezo wa soka unavyoelekeza.
Kwa mujibu wa Jackson, kwa kudhihirisha hilo baada Kocha msaidizi huyo kutolewa kwenye benchi na mwamuzi, alisikika akiwahamasisha wachezaji wake kwa kusema:”Wagongeni tu hao”, na hicho ndicho kilichotokea.
Alisema wameumizwa sana na aina isiyofaa ya uchezaji iliyoonyeshwa na wachezaji wa Rhino na pia wanasikitika kuona aina hiyo ya uchezaji inafumbiwa macho wakati wao (Mbeya City), wanaamini nidhamu ndio ushindi.
Aliziomba mamlaka zote zinazohusika na Ligi Kuu ya Tanzania Bara,maarufu zaidi Ligi ya Vodacom (VPL),waitazame upya mechi hiyo ili kulinda nidhamu ya Ligi Kuu na kutoa maamuzi sahihi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment