'
Friday, March 14, 2014
TAMBWE HAUZWI NG'O-SIMBA
UONGOZI wa klabu ya Simba umesema hauna mpango wa kumuuza mshambuliaji wake nyota, Hamisi Tambwe kwa bei yoyote.
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, Tambwe ana mkataba wa kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili.
Kamwaga alisema hayo kutokana na baadhi ya magazeti kuripoti jana kuwa, mchezaji huyo yupo tayari kujiunga na Yanga iwapo atalipwa mshahara mnono.
"Tambwe amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili, hivyo hatuwezi kumuuza kwa klabu yoyote kwa sasa,"alisema.
Tambwe, ambaye ni raia wa Burundi, alitia saini mkataba wa kuichezea Simba mwaka jana, mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspope na aliyekuwa katibu mkuu, Evodius Mtawala.
Kabla ya kujiunga na Simba, Tambwe alikuwa akiichezea klabu ya Vital'O ya Burundi, ambaye aliiwezesha kutwaa Kombe la Kagame mwaka jana nchini Sudan na kuibuka kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo.
Kwa sasa, Tambwe anaongoza kwa ufungaji mabao katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, akiwa amefunga mabao 19.
Wakati huo huo, uongozi wa Simba umesema, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Zdravko Logarusic, atamaliza mkataba wake wa kuifundisha timu hiyo 31 Mei mwaka huu.
Kamwaga alisema jana kuwa, bado hawajawa na uhakika wa kumuongezea mkataba kocha huyo kwa vile hatima yake itaamuliwa na kamati ya utendaji ya Simba, itakayopitia mwenendo wa timu hiyo katika ligi kuu msimu huu.
Loga alikabidhiwa jukumu la kuinoa Simba baada ya kutimuliwa kwa kocha mkuu wa zamani, Abdalla Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo 'Julio'.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment