'
Monday, March 17, 2014
YANGA, MTIBWA HAKUNA MBABE, AZAM YAIGAGADUA COASTAL UNION
NA FRED MAJALIWA, MOROGORO
MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga jana walishindwa kuonyesha makeke yao mbele ya Mtibwa Sugar, baada ya kulazimishwa kutoka nayo suluhu katika mechi kali na ya kusisimua iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Yanga tangu iliporejea nchini Jumatatu iliyopita kutoka Misri baada ya kutolewa na Al Ahly katika raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika.
Sare hiyo imeiwezesha Yanga kurejea nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kati yake na Mbeya City, ambayo imeshuka nafasi ya tatu.
Yanga inazo pointi 39 baada ya kucheza mechi 18 sawa na Mbeya City yenye idadi hiyo ya pointi baada ya kucheza mechi 21. Yanga imefunga mabao 41 na kufungwa 12 wakati Mbeya City imefunga mabao 27 na kufungwa 17.
Washindi wa pili wa ligi hiyo, Azam wameendelea kujichimbia kileleni mwa ligi hiyo baada ya kuichapa Coastal Union mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Chamazi ulioko Mbagala, Dar es Salaam. Ushindi huo umeiwezesha Azam kuwa na pointi 43 baada ya kucheza mechi 19.
Yanga ililianza pambano hilo kwa kasi na kulifikia lango la Mtibwa dakika ya kwanza wakati Emmanuel Okwi alipopiga mpira kichwa ukatumbukia ndani ya eneo la hatari na kumkuta Nizar Khalfan, lakini shuti lake lilimlenga kipa Hussein Sharrif.
Katika dakika ya nane na tisa, Mtibwa ilifanya mashambulizi makali kwenye lango la Yanga huku ikishangiliwa na mashabiki wa Simba na kupata kona mbili, lakini hazikuweza kuzaa matunda.
Kiungo Shaaban Nditi alikuwa nyota ya mchezo kwa Mtibwa katika dakika za mwanzo za pambano hilo kutokana na kutawala dimba la kati huku akirudi nyuma kusaidia kuokoa mashambulizi.
Okwi nusura aipatie bao Yanga dakika ya 20 alipounganisha kwa kichwa krosi kutoka pembeni ya uwanja, lakini mpira ulikwenda moja kwa moja mikononi mwa kipa Sharrir.
Dakika moja baadaye, Okwi na Didier Kavumbagu walijichanganya ndani ya eneo la hatari la Mtibwa wakiwa wamebaki ana kwa ana na kipa Sharrif, Okwi akapiga shuti dhaifu lililodakwa na kipa huyo.
Mtibwa ilipata nafasi nzuri dakika ya 26 baada ya mwamuzi Zakaria Jacob kutoka Pwani kuamuru ipigwe adhabu ndogo nje kidogo ya eneo la hatari la Yanga baada ya beki Juma Abdul kucheza rafu, lakini shuti la Shabani Kisiga liliokolewa na kipa Juma Kaseja.
Kipa Sharrif wa Mtibwa alilazimika kufanyakazi ya ziada dakika ya 38 kuokoa mpira mrefu kwa kichwa na kutua kwa Okwi wa Yanga, aliyekuwa akijiandaa kufunga, lakini akaukosa.
Lango la Yanga lilikuwa kwenye kimbembe dakika ya 43 na 45, lakini mabeki wake wakiongozwa na Kelvin Yondan na Nadir Haroub, walisimama imara kuondosha hatari hizo. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Kipindi cha pili kilianza kwa kosi kwa Mtibwa baada ya mshambuliaji wake, Abdalla Juma kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Jacob kwa kosa la kumpiga kichwa beki Yondan wa Yanga.
Didier Kavumbagu aliikosesha Yanga bao dakika ya 71 baada ya kushindwa kuunganisha wavuni krosi maridadi iliyopigwa na Okwi kutoka pembeni ya uwanja.
Dakika 10 baadaye, Kavumbagu alishindwa kuukwamisha mpira wavuni baada ya kupenyezewa pasi akiwa ndani ya eneo la hatari huku kipa Sharrif akiwa ametoka langoni. Shuti lake lilipaa juu ya langu.
Hussein Javu, aliyeingia kipindi cha pili badala ya Hamisi Kiiza, angeweza kufunga bao dakika ya 83 alipopewa pasi akiwa nje kidogo ya eneo la hatari, lakini shuti lake lilitoka pembeni ya lango.
Yanga itabidi waijutie nafasi waliyoipata dakika ya 91 baada ya Okwi kuingia na mpira ndani ya 18, lakini shuti lake liligonga mwamba wa goli na mpira kurudi uwanjani, ambako uliokolewa na mabeki wa Mtibwa.
Yanga: Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondan, Nadir Haroub, Frank Domayo, Simon Msuva, Nizar Khalfan, Hassan Dilunga, Emmanuel Okwi, Didier Kavumbagu, Hamisi Kiiza/Hussein Javu.
Mtibwa: Hussein Sharrif, Hassan Ramadhani, Paulo Ngelema, Dickson Daudi, Salum Mbonde, Shaabani Nditi, Ally Shomari/Saidi Mkopi, Abdalla Juma, Mohamed Mkopi na Vicent Barnabas/Jamal Mnyate.
Wakati huo huo, mabao yaliyofungwa na Kipre Tcheche na John Bocco jana yaliiwezesha Azam kuinyuka Coastal Union mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi.
Tchetche alifunga bao la kwanza dakika ya 23 kabla ya kuongeza la pili dakika ya 38. Bao la tatu lilifungwa na John Bocco dakika ya 64 wakati la nne lilifungwa na Kevin Friday dakika ya 90.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment