KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, March 2, 2014

SIMBA YATULIZA MZUKA, TAMBWE AFIKISHA MABAO 19


SIMBA jana iliwapa furaha mashabiki wake baada ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 3-2 katika mechi ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo uliiwezesha Simba kuendelea kushika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 33, nyuma ya vinara Yanga wanaoongoza kwa kuwa na pointi 40, wakifuatiwa na Azam yenye pointi 30 na Mbeya City yenye pointi 36.

Mshambuliaji Hamisi Tambwe aliendelea kudhihirisha ukali wake katika kupachika mabao wavuni baada ya kuifungia Simba mabao mawili kati ya matatu. Bao lingine lilifungwa na Haruna Chanongo.

Tambwe aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya 23 kwa mkwaju wa adhabu baada ya beki mmoja wa Ruvu Shooting kumchezea rafu Jonas Mkude nje kidogo ya eneo la hatari.

Mrundi huyo aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 32 baada ya kumtoka beki Hamisi Kisuke wa Ruvu Shooting na kufumua shuti lililomshinda kipa Abdalla Rashid. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.

Ruvu Shooting ilipata bao la kwanza dakika ya 74 kupitia kwa Saidi Dilunga baada ya kuunganisha mpira wa kona uliopigwa na Michael Aidan.

Chanongo aliifungia Simba bao la tatu dakika ya 76 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Amri Kiemba kabla ya Ruvu kuongeza bao la pili dakika ya 83 lililofungwa na Jerome Lembele kwa njia ya penalti baada ya beki mmoja wa Simba kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

No comments:

Post a Comment