LONDON, England
HATIMAYE mshambuliaji, Olivier Giroud wa klabu ya Arsenal ameamua kuvunja ukimya kwa kujibu tuhuma za kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamitindo, Celia Kay.
Giroud anatuhumiwa kumpeleka Kay kwenye hoteli ya Four Seasons iliyoko Canary Wharf siku moja kabla ya Arsenal kuichapa Crystal Palace katika mechi ya ligi kuu ya England iliyochezwa Februari 2 mwaka huu.
Kocha Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger, hadi sasa hajaamua kuweka wazi kuhusu hatua zitakazochukuliwa kwa Giroud baada ya kukiri kufanya mapenzi na binti huyo wakati akiwa katika majukumu ya kuitumikia timu yake.
Wenger alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa, suala la mchezaji huyo ni la ndani na litashughulikiwa na uongozi wa klabu.
"Hili ni suala la ndani, sitaki kulizungumza hadharani kwa sababu naheshimu maisha yake binafsi,"alisema Wenger.
Kay alimpiga picha Giroud alipokuwa kwenye chumba cha hoteli hiyo, akiwa amevaa chupi ya ndani na kuisambaza kwenye mitandao, ukiwemo mtandao wa MailOnline.
Awali Giroud, ambaye aliifungia Arsenal mabao mawili ilipoichapa Everton mabao 4-1 katika mechi ya Kombe la FA iliyochezwa wiki iliyopita, alitoa taarifa ya kuomba msamaha kwa mkewe, Jennifer na Wenger.
"Naomba radhi kwa mke wangu, familia yangu, marafiki, kocha, wachezaji wenzangu na mashabiki,"alisema Giroud.
"Napaswa kuipigania familia na klabu yangu na kuomba radhi kwao," alisema mshambuliaji huyo.
"Kuna mambo yaliyokuwa na ukweli, lakini mengine yalikuwa ya uongo. Lakini hayo yamepita kwa sasa,"alisema nyota huyo wa Arsenal, ambaye Juni mwaka jana mkewe alijifungua mtoto wa kiume.
"Kitu ambacho hakiwezi kuniua, kinanifanya niwe jasiri. Nashawishika kuamini kwamba, kina kinachotokea kwangu, kitanifanya niwe na nguvu zaidi,"aliongeza.
Giroud alisema anachopaswa kukifanya kwa sasa ni kuelekeza nguvu na akili yake uwanjani kwa kuitumikia vyema klabu yake na kutunza familia yake.
"Kilikuwa kipindi kigumu. Unapaswa kuwa na ujasiri kichwani kwako. Nilitumia mchezo wa soka kupambana na hili. Mchango wa Kocha Arsene Wenger ulikuwa muhimu. Nilizungumza naye.
"Nataka kusahau kuhusu hili kwa sasa na kuendelea na mambo mengine na kuanza upya,"alisisitiza.
Arsenal ilipanga kumtoza faini ya pauni 230,000 mchezaji huyo, lakini baadaye iliamua kumuunga mkono baada ya kukanusha tuhuma hizo. Wanasheria wa mchezaji huyo nao wameliandikia barua gazeti la Daily Mail kulilaumu kwa kuandika habari hizo.
No comments:
Post a Comment