KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 5, 2014

SIMBA, PRISONS KAZI IPO JUMAPILI


KOCHA Mkuu wa Simba, Logarusic akitoa maelekezo kwa wachezaji wake katika moja ya mechi za timu hiyo.
TIMU kongwe ya soka nchini, Simba mwishoni mwa wiki hii itakuwa na kibarua kigumu itakapomenyana na Prisons katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Pambano hilo litakalochezwa Jumapili, linatarajiwa kuwa na ushindani mkali kwa vile kila timu itapania kushinda ili kujiimarisha kwenye nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo.

Simba inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 35 baada ya kucheza mechi 20, nyuma ya vinara Azam wenye pointi 40, wakifuatiwa na mabingwa watetezi Yanga wenye pointi 38 na Mbeya City yenye pointi 36. Prisons ni ya 10 ikiwa na pointi 21.

Simba itacheza mechi hiyo siku chache baada ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ushindi ambao uliwapa ahueni mashabiki wa klabu hiyo baada ya kuiona timu yao ikivurunda katika mechi tatu mfululizo.

Jahazi la Simba lilianza kusuasua baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro, ikachapwa bao 1-0 na Mgambo JKT mjini Tanga, ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbeya City mjini Mbeya kabla ya kuchapwa mabao 2-1 na JKT Ruvu.

Ofisa Habari wa Simba, Asha Muhaji alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, kikosi chao kinatarajiwa kuondoka Dar es Salaam leo kwa basi kwenda Mbeya kwa ajili ya mechi hiyo.

Asha alisema wachezaji wote wa timu hiyo wapo fiti na wana ari kubwa ya kuendeleza wimbi la ushindi baada ya kuifunga Ruvu Shooting mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zitakazochezwa keshokutwa, Mbeya City itaikaribisha Rhino Rangers mjini Mbeya, Ruvu Shooting itacheza na JKT Oljoro kwenye uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati Ashanti watakuwa wageni wa Coastal Union mjini Tanga.

No comments:

Post a Comment