KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, March 7, 2014

WAMISRI WAIFANYIA KITU MBAYA YANGA, MECHI YAHAMISHIWA ALEXANDRIA



KIKOSI cha wachezaji na viongozi wa Yanga kikiwa kwenye hoteli ya Nile mara baada ya kuwasili mjini Cairo, Misri. 
HUU ndio uwanja wa Border Guard, unaomilikiwa na klabu ya Haras El Hodood, ambao utatumika kwa ajili ya mechi ya Yanga na Al Ahly.

NA BARAKA KAZUGUTO, CAIRO
HATIMAYE pambano la marudiano la raundi ya pili ya michuano ya soka ya klabu bingwa Afrika kati ya Yanga ya Tanzania na Al Ahly ya Misri sasa litafanyika kwenye Uwanja wa Border Guard ulioko katika mji wa Alexandria.

Taarifa iliyotolewa na Chama cha Soka cha Misri jana ilieleza kuwa, pambano hilo litakalofanyika kesho usiku, limehamishiwa Alexandria baada ya Jeshi la Misri kugoma uwanja wake ulioko mjini Cairo kutumika kwa ajili ya mechi hiyo.

Mji wa Alexandria upo kilometa 200 kutoka Cairo, ambako kikosi cha Yanga kimeweka kambi kwenye hoteli ya Nile Paradise Inn baada ya kuwasili mjini hapa juzi asubuhi.

Uwanja wa Border Guard unamilikiwa na klabu ya Haras El-Hodod ya Misri na kwa kawaida, una uwezo wa kuchukua mashabiki 22,500.
Yanga imetua Misri ikiwa na msafara wa watu 31, wakiwemo wachezaji 18 na kupokewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mohamed Hamza.

Baada ya kupata taarifa hizo kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Misri, uongozi wa Yanga chini ya Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga, umeanza maandalizi kwa lengo la kuhakikisha kikosi cha timu hiyo kinakwenda Alexandria kwa ndege badala ya kusafirishwa kwa basi.

Sanga alisema jana mjini hapa kuwa, wameshangazwa kuona taarifa za mahali, ambako mchezo huo utachezwa, zinatolewa siku tatu kabla ya mchezo wakati kiutaratibu zinatakiwa kutolewa wiki moja.

"Viongozi wa Al Ahly walipokuja Tanzania wiki mbili zilizopita, walisema mchezo wa marudiano utachezwa Cairo, lakini tunashangaa kusikia wamebadili uwanja na sasa tutacheza nao Alexandria,"alisema.

Licha ya kufanyika kwa mabadiliko hayo, Sanga alisema wamejiandaa vyema kukabiliana na wapinzani wao na wana uhakika mkubwa wa kushinda mchezo huo na kuweka rekodi ya kuivua ubingwa timu hiyo ya Misri.

Kwa mujibu wa taarifa ya Chama cha Soka cha Misri, pambano kati ya Yanga na Al Ahly litachezwa bila ya kuwepo kwa watazamaji uwanjani kwa hofu ya kutokea vurugu.

Katika mchezo wa awali, uliochezwa wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, Yanga iliichapa Al Ahly bao 1-0, lililofungwa kwa kichwa na beki Nadrir Haroub 'Cannavaro', akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Simon Msuva.

Wakati huo huo, washambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza na Emmanuel Okwi, wamewasili mjini Cairo na kujiunga na wenzao kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo.

Okwi na Kiiza waliwasili Cairo saa saba usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri, wakitokea Zambia, ambako walikwenda kuichezea timu yao ya taifa katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Zambia.

No comments:

Post a Comment