SERIKALI imesema ipo kwenye hatua za mwisho katika mchakato wa kuipatia klabu ya Yanga kibali cha nyongeza katika eneo la Jangwani kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa kisasa wa soka.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira katika Manispaa ya Ilala, Sultan Salim, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamelipa kipaumbele kikubwa ombi hilo la Yanga na kusisitiza kuwa, mambo yatakuwa mazuri.
Sultan alisema hayo baada ya jopo la madiwani na wajumbe wa kamati yake, kutembelea makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam na kukagua eneo, ambalo klabu hiyo inataka iongezwe kwa ajili ya ujenzi huo.
"Yanga wamekuwa wa kwanza kupewa kipaumbele kikubwa kuliko wote. Tulipokea maombi mengi, lakini hili la Yanga limepewa umuhimu mkubwa na mara baada ya ziara hii leo, tutakutana ili kutoa uamuzi kuhusu ombi lao,"alisema Sultan.
Alisema watalitolea uamuzi ombi hilo baada ya kutembelea eneo, ambalo Yanga wanalihitaji kwa ajili ya kupanua ujenzi wa uwanja wa kisasa pamoja na majengo mengine ya kibiashara.
Sultan alisema baada ya kamati yake kujadili ombi hilo, itatuma wataalamu wake kwenye eneo hilo kwa ajili ya ukaguzi wa mwisho kabla ya kutoa kibali cha kuiruhusu Yanga kuanza ujenzi huo.
Mjumbe wa Bodi ya Udhamini ya Yanga, Francis Kifukwe, alisema wanaishukuru Manispaa ya Ilala kwa kutuma ujumbe huo kwenda kukagua eneo wanalolihitaji kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wao.
"Sasa hivi tunavuta tu subira kwa sababu tunaamini mambo yatakuwa mazuri kwani kila kitu kuhusiana na ujenzi huo kimeshapangwa na tayari tunazo pesa za kuanzia ujenzi huo,"alisema Kifukwe.
Alisema endapo serikali itawapa kibali cha kuanza ujenzi huo, wanatarajia kuanza kazi hiyo ndani ya miezi sita.
Yanga inahitaji nyongeza ya eneo la hekta 11 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo wa kisasa ambapo kwa sasa eneo linalomilikiwa na klabu hiyo ni hekta 3.5.
Januari mwaka jana, uongozi wa Yanga uliitangaza Kampuni ya Beinjing Cosntruction Engineering Group (BCEG) ya China, iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuwa ingeanza ujenzi wa uwanja huo Mei mwaka jana.
Hata hivyo, ujenzi huo ulichelewa kuanza kutokana na Yanga kuhitaji eneo la ziada la hekta 11.5.
Uwanja huo, ambao utapewa jina la Jangwani City, utakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 40,000 waliokaa kwenye viti, huku ukiwa na sehemu za maegesho ya magari, watu maarufu (VIP), hospitali, hoteli na hosteli.
No comments:
Post a Comment