Wachezaji wa Yanga wakipongezana baada ya kupata bao la ushindi dhidi ya Al Ahly ya Misri. Kutoka kushoto ni mfungaji wa bao hilo, Nadir Haroub 'Cannavaro', Emmanuel Okwi na Simon Msuva. (Picha kwa hisani ya blogu ya Bin Zubeiry).
BAO lililofungwa na beki Nadir Haroub 'Cannavaro' jana liliiwezesha Yanga kuweka historia ya kuifunga Al Ahly ya Misri kwa mara ya kwanza katika michuano ya klabu bingwa Afrika.Kabla ya ushindi huo wa jana, Yanga ilikuwa haijawahi kuifunga timu yoyote ya Misri katika michuano hiyo. Ilitolewa mara tatu na Al Ahly kwa kufungwa idadi kubwa ya mabao.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya mashabiki, Cannavaro alifunga bao hilo la pekee kwa kichwa, akiunganisha wavuni kona iliyopigwa na Simon Msuva.
Kuingia kwa bao hilo kuliamsha shangwe na hoi hoi kutoka kwa mashabiki wa Yanga, ambao licha ya timu yao kufanya mashambulizi mengi na kupata nafasi zaidi ya 10 za kufunga mabao, hawakuwa na uhakika wa ushindi.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Cannavaro alisema ameamua kumzawadia bao hilo mkewe, kwa kuwa ni la kihistoria kwake na klabu ya Yanga.
Al Ahly ilicheza mechi hiyo kwa kasi ndogo na kufanya mashambulizi machache ya kushtukiza, lakini hayakuwa na madhara yoyote kwa kipa Deogratius Munishi 'Dida', kutokana na ukuta imara uliowekwa na mabeki Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Cannavaro na kiungo Frank Dumayo.
Iwapo washambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi, Mrisho Ngasa, Hamisi Kiiza na Msuva wangekuwa makini kila walipofika kwenye lango la Al Ahly, wawakilishi hao wa Tanzania wangetoka uwanjani na lundo la mabao.
Lakini papara za washambuliaji hao, kutokuwa makini na kujiamini, kuliwafanya wapoteze nafasi nyingi za kufunga mabao huku Wamisri wakionekana dhahiri kuchanganyikiwa kutokana na kasi ya mashambulizi yaliyokuwa yakipelekwa kwenye lango lao.
Timu hizo mbili zinatarajiwa kurudiana wiki ijayo mjini Cairo, Misri na Yanga wanatarajiwa kuondoka nchini kati ya keshokutwa na Alhamisi. Ili isonge mbele katika michuano hiyo, Yanga inahitaji sare ya aina yoyote wakati Al Ahly italazimika kushinda mabao 2-0.
Makamu Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya kimataifa ya Yanga, Abdalla Bin Kleb alisema jana kuwa, wamepanga kumtanguliza mtu mmoja mjini Cairo kwa ajili ya kuandaa mazingira mazuri pamoja na mahali, ambako timu hiyo itafikia.
Upo uwezekano mkubwa kwa pambano hilo la marudiano kuchezwa bila mashabiki, kufuatia vurugu zilizotokea wiki mbili zilizopita katika mechi kati ya Al Ahly na Esperance ya Tunisia.
Yanga: Deogratius Munishi 'Dida', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Nadir Haroub 'Cannavaro', Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, Mrisho Ngasa, Hamizi Kiiza/Didier Kavumbagu.
No comments:
Post a Comment