KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 20, 2014

MZIMU WA PENALTI WAITESA YANGA




MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka yaTanzania Bara, Yanga jana walizidi kupunguzwa kasi ya kuwania ubingwa huo msimu huu baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Azam.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 14 lililofungwa na Didier Kavumbagu kabla ya Kelvin Friday kuisawazishia Azam dakika ya 84.

Kutokana na matokeo hayo, Azam inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 44 baada ya kucheza mechi 20, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 40 baada ya kucheza mechi 19.

Sare hiyo ilikuwa ya pili mfululizo kwa Yanga tangu ilipotolewa na Al Ahly ya Misri katika michuano ya klabu bingwa Afrika. Wiki iliyopita, mabingwa hao watetezi walilazimishwa kutoka suluhu na Mtibwa Sugar mjini Morogoro.

Kavumbagu aliifungia Yanga bao la kuongoza baada ya kumalizia mpira uliotemwa na kipa wa Azam, Aishi Manula, kufuatia krosi iliyopigwa na Simon Msuva kutoka pembeni ya uwanja.

Friday aliisawazishia Azam kwa shuti kali baada ya mabeki wa Yanga kuzembea kuondosha mpira kwenye lango lao. Jitihada za kipa Juma Kaseja kuokoa shuti hilo hazikuzaa matunda.

Yanga ililianza pambano hilo kwa kasi na kupata nafasi nzuri ya kuongeza bao dakika ya 15 wakati Simon Msuva alipopewa pasi akiwa ndani ya 18, lakini shuti lake lilitoka nje.

Mshambuliaji Kipre Tchetche wa Azam alikuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Yanga kutokana na kuisumbua ngome yao mara kwa mara. Mshambuliaji huyo kutoka Ivory Coast nusura afunge bao dakika ya 22, lakini shuti lake liligonga mwamba na mpira kurudi uwanjani.

Kavumbagu nusura afunge bao lingine dakika ya 25 baada ya kusogezewa mpira nje kidogo ya eneo la hatari, lakini shuti lake lilidakwa kwa ustadi mkubwa na kipa Aishi Manula wa Azam.

Yanga ilifanya shambulizi lingine la nguvu dakika ya 30 wakati Emmanuel Okwi, alipoitoka ngome ya Azam na kupiga mkwaju mkali akiwa nje ya eneo la hatari, lakini mpira ulipanguliwa na kipa Manula. Timu hizo zilikwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0.

KIPINDI CHA PILI
Azam iliongeza kasi ya mchezo kipindi cha pili na nusura ipate bao dakika ya 50 wakati Kelvin Friday alipomalizia kazi nzuri iliyofanywa na Tchetche, lakini shuti lake lilitoka pembeni ya lango.

Yanga ilipata adhabu ya penalti dakika ya 69 iliyolewa na mwamuzi Hashim Abdalla baada ya beki mmoja wa Azam kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari, lakini shuti la Kiiza lilitoka nje.

Azam ilipata pigo dakika ya 73 baada ya mwamuzi Hashim kumtoa nje kwa kadi nyekundu beki Erasto Nyoni kwa kosa la kumtolea lucha chafu. Awali, Nyoni alilimwa kadi ya njano

REKODI
Mechi hiyo ilikuwa ya 12 kwa Yanga kukutana na Azam kwenye michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara. Katika mechi hizo, Yanga imeshinda mitano wakati Azam imeshinda minne huku mechi mbili wakitoka sare.

Nje ya ligi kuu, timu hizo zimekutana mara tano, Yanga imeshinda mara mbili (Ngao ya Hisani na Kombe la Kagame) wakati Azam imeshinda mara tatu (Kombe la Mapinduzi na mechi za kirafiki).

John Bocco ndiye mchezaji aliyefunga magoli mengi zaidi katika mechi kati ya Yanga na Azam wakati Nadir Haroub 'Canavaro' anashikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi.

Yanga SC: Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Didier Kavumbangu/Mrisho Ngasa, Hamisi Kiiza/Hussein Javu na Emmanuel Okwi.

Azam: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gabriel Michael, Saidi Mourad, David Mwantika, Kipre Balou, Himid Mao, Salum Abubakari, John Bocco, Kipre Tchetche na Khamisi Mcha/ Kelvin Friday.

No comments:

Post a Comment