'
Friday, March 14, 2014
NGASA, NIYONZIMA KUIKOSA MTIBWA LEO
MSHAMBULIAJI Mrisho Ngassa na kiungo Haruna Niyonzima wa Yanga, wataikosa mechi ya leo ya ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, Ngasa na Niyonzima wataikosa mechi hiyo kutokana na kuwa majeruhi.
Yanga inatarajiwa kushuka dimbani leo kukipiga na Mtibwa Sugar katika mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Mabingwa hao watetezi wa Tanzania Bara, walirejea nchini jana saa 12 asubuhi wakitokea Cairo, Misri, ambako walikwenda kurudiana na Al Ahly katika mechi ya raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika.
Katika mechi hiyo iliyochezwa mjini Alexandria, Yanga ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1, kufuatia Al Ahly kushinda bao 1-0.
Kwa mujibu wa Mkwasa, Ngasa huenda akakaa nje ya uwanja kwa wiki moja kutokana na kupata majeraha makubwa wakati wa mechi hiyo, ambapo alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Athumani Iddi 'Chuji'.
Kwa upande wa Niyonzima, alisema mchezaji huyo bado anasumbuliwa na ugonjwa wa malaria, uliosababisha ashindwe kucheza mechi hiyo ya marudiano dhidi ya Wamisri.
Licha ya kukosekana kwa nyota hao, Mkwasa alisema kikosi chake kipo vizuri na kimejiandaa vyema kushinda mechi yao dhidi ya Mtibwa Sugar.
"Kuanzia sasa, nguvu zetu tumezielekeza kwenye mchezo wa Jumamosi na uongozi utatoa taarifa ni lini timu itakwenda Morogoro kwa ajili ya mchezo huo,"alisema Mkwasa.
Kocha huyo alisema kikosi chake kilitarajiwa kuendelea na mazoezi jana jioni katika uwanja wa Kaunda ulioko makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam na huenda wakaenda Morogoro leo mchana au kesho asubuhi.
"Kiufundi tumejipanga kuhakikisha tunashinda mchezo wetu na Mtibwa ili tujiweke katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu, hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa tupo nafasi ya tatu lakini tunaamini tutarejea kileleni,"alisema Mkwasa.
Yanga inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 38 kutokana na mechi 17 ilizocheza, nyuma ya Mbeya City yenye pointi 39 baada ya kucheza mechi 21. Azam inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na ponti 40.
Mabingwa hao watetezi wanakabiliwa na mechi nyingine ngumu Machi 19 mwaka huu dhidi ya Azam, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment