MADRID, Hispania
MSHAMBULIAJI Gareth Bale amemwelezea nyota mwenzake wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, kuwa ndiye mchezaji bora duniani kwa sasa na ataiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa Hispania msimu huu.
Licha ya Lionel Messi kuonyesha kiwango cha juu wakati Barcelona ilipomenyana na Manchester City katika mechi ya ligi ya mabingwa wa Ulaya Jumatano iliyopita, Bale amesema ana hakika Ronaldo yupo kwenye kiwango bora zaidi.
"Cristiano ni mchezaji bora duniani kwa sasa na sote tunaelewa jinsi alivyo mzuri,"amesema Bale.
"Huwa inanisaidia sana ninapocheza safu ya ushambuliaji pamoja na Ronaldo na natumaini tutacheza vizuri zaidi na kushinda taji hili msimu huu,"ameongeza.
Bale alikuwa akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa viatu vyake vipya vya Adidas F50 iliyofanyika mjini hapa.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Tottenham ya England alishindwa kujizuia kuzungumzia mafanikio, ambayo Real Madrid inaweza kuyapata mwishoni mwa msimu huu.
Madrid inatarajiwa kumenyana na Barcelona, Machi 23 mwaka huu katika mechi ya ligi ya Hispania, inayotarajiwa kuwa na ushindani mkali na wa aina yake.
"Kuna mechi za kufurahisha kwa mchezaji yeyote. Tuna hamu ya kupambana nao, na kama inawezekana kuwafunga. Mechi ijayo tutacheza dhidi ya Malaga, hivyo tumeelekeza nguvu zetu katika mechi hizo kwa sasa,"alisema Bale.
Nyota huyo wa Real Madrid amesema, lengo la Madrid msimu huu ni kutwaa mataji yote matatu wanayoshindania na kwamba wanayo nafasi kubwa ya kufanya hivyo, lakini wanapaswa kwenda hatua kwa hatua.
Kwa sasa, Madrid inaongoza ligi ya Hispania kwa tofauti ya pointi tatu na Atletico Madrid, inayoshika nafasi ya pili. Timu zote mbili zimesaliwa na michezo 11. Madrid inaongoza kwa kuwa na pointi 67, Atletico inazo pointi 64 wakati Barcelona ni ya tatu ikiwa na pointi 63.
"Ni kweli kwamba tupo kwenye nafasi nzuri,"alisema Bale. "Kama tutaendelea kufanya kazi nzuri na kushinda, hatuna sababu ya kuwa wasiwasi kuhusu timu zingine na tunaweza kutimiza malengo yetu, ambayo ni kutwaa ubingwa wa ligi,"amesema Bale.
Nyota huyo wa Madrid amesema, kwa kipindi cha miezi sita alichoichezea timu hiyo, amekuwa akivutiwa na mbinu za hali ya juu za kisoka katika ligi ya Hispania.
Madrid inatarajiwa kushuka dimbani Alhamisi ijayo kukipiga na Schalke ya Ujerumani katika mechi ya marudiano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya baada ya kuibwaga timu hiyo kwa mabao 6-1. Mabao ya Madrid yalifungwa na Bale, Ronaldo na Karim Benzema, kila mmoja akitupia mawili.
Bale amesema wanayo nafasi nzuri ya kutwaa taji hilo la Ulaya iwapo watavuka hatua za awali na kuwa na bahati.
"Kwa sasa bado zipo timu ngumu katika ligi ya mabingwa. Sidhani kama ipo inayopewa nafasi kubwa zaidi kuliko zingine,"alisema.
No comments:
Post a Comment