KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, October 24, 2012

ABDALLA KIBADENI: WAAMUZI WANATUHARIBIA ULAJI


JINA la Abdalla 'King' Kibadeni si geni masikioni mwa mashabiki wa soka nchini. Ni mmoja wa wachezaji waliong'ara miaka ya 1970 akiwa na kikosi cha Simba na timu ya taifa, Taifa Stars. Kwa sasa Kibadeni ni Kocha Mkuu wa Kagera Sugar ya Bukoba. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na ATHANAS KAZIGE  gazeti la Burudani, kocha huyo anazungumzia mambo mbali mbali kuhusu soka.

SWALI: Umekuwa kocha wa Kagera Sugar kwa kipindi kifupi, lakini umeiwezesha kupata mafanikio kwa kuifunga Yanga na kutoka sare na Simba katika mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara. Unaweza kutueleza nini siri ya mafanikio yako?
JIBU: Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kufanyakazi yangu kwa mafanikio. Lakini ukweli ni kwamba mafanikio yetu katika ligi yametokana na mambo mengi. Kubwa ni wachezaji kucheza kwa kujituma na kufuata maelekezo ya mwalimu na pia kuwemo kwa umoja miongoni mwa wachezaji na viongozi.
SWALI: Ni tatizo lipi kubwa, ambalo hadi sasa mmekuwa mkikumbana nalo mara kwa mara katika michuano ya ligi kuu?
JIBU: Tatizo kubwa ni uamuzi mbovu. Kusema kweli uamuzi katika mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara naweza kusema unatia kinyaa. Waamuzi wengi wamekuwa wakitoa maamuzi mabovu, iwe kwa makusudi kwa lengo la kuzibeba baadhi ya timu ama kutofahamu vyema sheria 17 za soka.
Japokuwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) limeweka waangalizi katika mechi zote za ligi, sidhani kama hilo litasaidia kitu. Na kama waangalizi hao wataweza kufanyakazi yao kwa umakini, nina hakika waamuzi wengi watafungiwa kwa vile wamekuwa wakifanya vitendo vingi vya ajabu.
Kila kukicha, makocha wengi wa timu za ligi kuu wamekuwa wakiwalalamikia waamuzi. Na si kwamba wanalalamika hivyo kwa lengo la kulinda vibarua vyao, huo ndio ukweli wenyewe.
SWALI: Unapenda kutoa mwito gani kwa TFF na waamuzi kuhusu tatizo hilo?
JIBU: Nawaomba wawe makini na kazi yao na waepuke vishawishi vya kuzibeba baadhi ya timu zenye uwezo kipesa. Wakifanya hivyo si tu kwamba wanazididimiza timu zisizokuwa na uwezo, bali pia wanautia doa mchezo wa soka na kujiharibia wao wenyewe.
Kibaya zaidi, iwapo wataendelea na uchezeshaji wao huo mbovu, ipo siku tutashuhudia mauaji kwenye viwanja vya soka kwa sababu utafika wakati mashabiki watasema tumechoka kuonewa, watachukua sheria mikononi. Litakuwa jambo la hatari sana.
Naishauri TFF ichukue tahadhari mapema kabla ya kutokea matukio ya aina hiyo. Na kama haitakuwa makini, itakuwa ni ndoto kwa Tanzania kutoa waamuzi wa kuchezesha fainali za Afrika ama Kombe la Dunia.
SWALI: Unayaonaje maendeleo ya Kagera Sugar hadi sasa? Kuna uwezekano wowote kwa timu yako kutwaa ubingwa wa ligi ama kushika moja ya nafasi tatu za kwanza?
JIBU: Namshukuru Mungu kwamba timu inaendelea vizuri kwa sababu hatupo kwenye nafasi mbaya katika msimamo wa ligi. Tumeweza kuifunga Yanga nyumbani na kutoka sare na Simba ugenini. Haya ni matokeo mazuri kwetu.
Hadi sasa sina mkataba na Kagera Sugar, nafanyakazi kwa makubaliano maalumu ama naweza kusema bado nipo chini ya uangalizi kwa miezi sita. Iwapo timu itafanya vizuri, huenda uongozi ukanipa mkataba.
Moja ya malengo niliyojiwekea pamoja na wachezaji wangu ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zetu zote za ligi na ikiwezekana tumalize msimu huu tukiwa katika moja ya nafasi tatu za kwanza.
SWALI: Je, umekuwa ukipata ushirikiano mzuri kutoka kwa msaidizi wako, Mrage Kabange na viongozi wa Kagera Sugar?
JIBU: Binafsi namshukuru sana Kabange, ambaye amekuwa akinipa ushirikiano mkubwa tangu nilipojiunga na timu hii. Pia nawashukuru wachezaji wote pamoja na viongozi kwa kunipa ushirikiano na kunifanya niifanye kazi yangu bila matatizo.
SWALI: Una maoni gani kuhusu uchaguzi mkuu ujao wa TFF?
JIBU: Umeniuliza swali zuri sana. Napenda kutumia fursa hii kuiomba kamati ya uchaguzi ya TFF kuwapima wagombea kwa mambo mbali mbali kabla ya kuwapitisha kuwania uongozi wa shirikisho hilo kwa sababu wengi hawana sifa na wamekuwa wakiwania uongozi kwa malengo yao binafsi, badala ya kuendeleza soka.
Na hili lifanyika kuanzia katika ngazi za wilaya na mikoa. Kusikuwepo nafasi ya kuwapitisha wagombea kwa sababu ya uwezo wao kifedha ama umaarufu wao. Wagombea wapitishwe kutokana na elimu zao, hasa za uongozi na uwezo wao.
Pengine ni vyema zingetolewa nafasi kwa watu waliowahi kucheza soka na kufika ngazi za juu kuwania uongozi katika ngazi zote zilizopo. Hawa angalau wanafahamu ABC ya soka kuliko wale, ambao hawajawahi kabisa kucheza mchezo huo.
SWALI: Unadhani tatizo hili la uongozi lipo kwenye vyama vya soka pekee?
JIBU: Hapana, tatizo hili lipo hata katika ngazi za klabu. Hata ukitazama klabu za Simba na Yanga, viongozi wake wengi sio watu wa mpira. Ni watu wanaotafuta umaarufu na kujinufaisha wao binafsi, ndio sababu matatizo katika klabu hizi hayaishi. Kila kukicha ni migogoro.
SWALI: Unatoa ushauri gani kwa serikali kuhusu maendeleo ya michezo nchini?
JIBU: Nawashauri viongozi wa serikali wahakikishe vyama vya kitaifa vya michezo vinatimiza malengo yake na viongozi wake wanaongoza kwa kufuata katiba. Hili litasaidia sana kuepusha migogoro

No comments:

Post a Comment