'
Wednesday, March 30, 2011
Yanga yanusa ubingwa
TIMU ya Yanga imeongeza kasi ya kuwania kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu, baada jana kuibanjua Azam FC mabao 2-1 katika mechi iliyokuwa na upinzani mkubwa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Matokeo hayo yamezidisha presha kwa Simba inayoshika usukani wa ligi hiyo kwani, Yanga sasa imefikisha pointi 43 ikibaki nafasi ya pili kwa kupitwa alama mbili na Simba. Timu hizo zote zimecheza mechi 20 na imebaki michezo miwili ligi kumalizika. Mshambuliaji John Bocco 'Adebayor' wa Azam FC alianza kutikisa nyavu za Yanga katika dakika ya nne ya mchezo huo baada ya kuunasa mpira kutoka kwa beki Chacha Marwa na kufunga bao kwa kumchambua kipa Ivan Knezevic.Kufungwa bao hilo kuliwaamsha Yanga ambao walilisakama lango la Azam kama nyuki na katika dakika ya 12 Jerry Tegete alikosa goli kutokana na shuti alilopiga kugonga mwamba na mpira kuokolewa na mabeki baada ya kurudi uwanjani. Tegete alifanya shambulizi hilo baada ya kupokea mpira wa krosi iliyopigwa na Davis Mwape, huku mchezaji huyo akikosa tena goli dakika ya 38 kufuatia shuti lake la mpira uliorushwa na Fred Mbuna, kupanguliwa na kipa wa Azam Vladimir Niyonkuru na kuwa kona butu.Dakika tatu kabla ya mapumziko Tegete aliisawazishia Yanga kwa mpira wa shuti kali baada ya kuunganisha krosi ya Shadrack Nsajigwa, huku mchezaji huyo akiwa shujaa kwa wana Jangwani baada ya kuongeza bao la pili dakika ya 60 kwa kuunganisha wavuni mpira uliotemwa na kipa Niyonkuru kufuatia kutema shuti kali la Davis Mwape.Kuingizwa kwa Kally Ongala kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Suleiman Kassim kulisaidia kuiimarisha Azam FC upande wa kiungo, lakini washambuliaji walishindwa kukwamisha mipira wavuni ikiwemo dakika ya 83, ambayo Boko apiga kichwa mpira na kutoka nje.Mrisho Ngasa, Tegete, na Nurdin Bakari walionyeshwa kadi za njano kwa utovu wa nidhamu.Akizungumzia matokeo hayo kocha wa Yanga, Sam Timbe, alisema kuwa wataendelea kupigana mpaka mechi ya mwisho kuwania ubingwa, huku kocha wa Azam, Stewart Hall akisema wamepoteza mchezo huo kwa sababu baadhi ya wachezaji wake tegemeo majeruhi na wengine wanasumbuliwa na uchovu wa safari ya timu ya taifa ya vijana iliyokwenda jijini Yaounde wiki iliyopita kucheza na Cameroon.Yanga: Ivan Knezevic, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Nadir Haroub 'Cannavaro', Chacha Marwa, Juma Seif/ Omega Seme, Fred Mbuna, Nurdin Bakari, Davis Mwape, Jerry Tegete, Kigi Makasi.Azam FC: Vladimir Niyonkuru, Ibrahim Shikanda, Malika Ndeule/Himid Mao, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Mutesa Mafisango, Mrisho Ngasa, Jabir Aziz, John Boko 'Adebayor', Ramadhani Chombo, Suleiman Kassim/Kally Ongala.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment