'
Thursday, April 7, 2011
Polisi kumwaga ajira kwa mastaa
UONGOZI wa timu ya soka ya Polisi Dodoma umepanga kumwaga ajira ya kudumu kwa wachezaji nyota ili kujenga kikosi imara msimu ujao. Katibu Mkuu wa timu hiyo, Leonard Kijangwa alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, kwa sasa wanasubiri ligi kuu ya Tanzania Bara imalizike kabla ya kuanza kutoa ajira hizo. Kijangwa alisema baada ya kumalizika kwa ligi hiyo, watakutana na viongozi wa benchi la ufundi kwa ajili ya kufanya tathimini ya ushiriki wa timu yao na pia kupitia mapendekezo ya Kocha John Simkoko. "Tumepanga kukutana mara ligi itakapomalizika,lengo letu ni kufanya usajili wa nguvu, lakini kwa kufuata mapendekezo na ushauri wa kocha wetu Simkoko,"alisema Kijangwa. Alisema wamejipanga vyema kusajili mchezaji yeyote, ambaye atapendekezwa na viongozi wa benhci la ufundi ili kuhakikisha wanakuwa na timu bora, ambayo msimu ujao itatoa ushindani mkali katika ligi kuu. Kijangwa alisema wamechoka kuiona timu hiyo ikiendelea kufanya vibaya katika ligi, hivyo dhamira yao kubwa ni kuwa na timu kali na yenye uwezo wa kutwaa ubingwa. "Nawaomba wachezaji wote wenye nia ya kucheza mpira, waondoke katika timu kubwa na kuja Polisi Dodoma ili waweze kupatiwa fomu za usajili na ajira ya kudumu kwani hata kama uwezo wao kisoka utaisha, wataendelea kuwepo katika ajira,"alisema Kijangwa. Habari zaidi zimeeleza kuwa timu hiyo imepanga kufanya mazungumzo na mshambuliaji wa Simba, Mbwana Samata na mastaa wengine ili kuwashawishi waweze kujiunga nao na timu hiyo na kupewa ajira.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment