KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 28, 2011

SHAMTE ALLY: Nipo tayari kucheza Yanga au Simba


WAKATI kipindi cha usajili kinatarajiwa kuanza rasmi mwezi ujao, kumekuwepo na habari nyingi kuhusu uhamisho wa wachezaji kutoka timu moja kwenda nyingine, akiwemo mshambuliaji Ally Shamte wa Yanga. Katika makala hii ya Mwandishi Wetu mchezaji huyo anaelezea kuhusu usahihi wa taarifa hizo na mikakati yake kisoka.

SWALI: Pole kwa kuumwa kwa kipindi kirefu na kusababisha ukaa nje ya dimba kwa muda mrefu.
JIBU: Asante sana.
SWALI: Kuna taarifa kwamba Yanga ina mpango wa kutaka kukuacha kwenye usajili wake msimu ujao, je kuna ukweli wowote kuhusu taarifa hizi?
JIBU: Ukweli ni kwamba mimi sina taarifa yoyote kuhusu kuachwa na klabu yangu ya Yanga. Kama jambo hilo lipo, inawezekana nitapatiwa taarifa hivi karibuni.
Lakini kama wamefanya hivyo, watakuwa wamenitendea jambo baya kwa sababu hawajui uwezo wangu kwa sasa upo vipi.
Licha ya jambo hilo, hata Kocha Sam Timbe hajawahi kuona uwezo wangu, sasa sijui wametumia vigezo gani kunitema. Kama kweli wamefanya hivyo, watanisikitisha sana. Lakini mimi sina taarifa yoyote.
SWALI: Mara ya mwisho kukutana na viongozi wa klabu ya Yanga ilikuwa lini na walikueleza jambo gani kuhusu hatma na mustakabali wako?
JIBU: Nilikutana na viongozi wangu kabla ya mchezo wa mwisho wa ligi kuu dhidi ya Toto African. Wakati huo timu ilikuwa inajiandaa na safari ya kwenda mkoani Mwanza.
Nategemea ndani ya wiki moja nitawasiliana nao ili kujua ukweli wa habari hizi na nini kinachofuata.
SWALI: Umewahi kukutana na kiongozi yeyote wa klabu ya Simba kwa siku za hivi karibuni?
JIBU: Wamekuja kuzungumza na mimi, lakini niliwaeleza kwamba nasubiri kujua hatma yangu ndani ya Yanga. Viongozi hao wamenipa muda ili niwape majibu.
Lakini nipo tayari kujiunga na timu hiyo endapo watanipa dau la nguvu ili niweze kucheza kwa vile mimi maisha yangu yanategemea soka na sio kitu kingine.
SWALI: Unajisikiaje kutokana na kushindwa kuichezea Yanga kwa muda mrefu?
JIBU: Najisikia vibaya sana kwani nilikuwa nimepanga malengo makubwa ndani ya msimu huu uliomalizika hivi karibuni, ikiwemo kucheza kwa kiwango cha hali ya juu.
Mbali na hayo, nilipanga kuhakikisha narejea katika kikosi cha kwanza cha Yanga huku nikisaka nafasi ya kuitwa kuichezea Taifa Stars.
Pia nilikuwa nawaza kusaka mbinu ya kupata timu ya kuchezea nje ya nchi ili niweze kuongeza kipato changu kwa vile maisha ya kucheza mpira ni mafupi sana.
SWALI: Una jambo gani ambalo ungependa kuwaeleza wachezaji wenzako wa Tanzania?
JIBU: Ninayo mambo mengi ya kuwaeleza wachezaji wenzangu pamoja na viongozi wa soka. Hivi sasa kumezuka tabia moja mbaya sana ndani ya klabu kubwa, hasa Simba na Yanga.
Wapo baadhi ya viongozi, ambao iwapo watatofautiana na mchezaji fulani, wanaanza kumjengea hoja au vitendo vya ajabu ili ashindwe a kutimiza majukumu yake.
Tabia hii ni mbaya sana. Napenda kuwaasa wachezaji wenzangu wajitume kwa nguvu zao zote na kujiweka pembeni na migogoro kwa vile inaweza kusababisha maafa kwao na familia zao kwa ujumla.
Nimewasikia baadhi ya wachezaji, ambao wapo Simba wanalalamika kuhusu kuwepo baadhi ya viongozi, ambao wanaendekeza chuki na wakati mwingine kutaka wachezaji fulani wasipangwe, kisa wana ugomvi na kiongozi fulani.
SWALI: Wewe binafsi unafikiri nini kifanyike ili kuondokana na tabia hiyo?
JIBU: Nawaomba viongozi hao wabadilike na kuwaacha wachezaji wapate nafasi ya kuzitumikia klabu zao na kuongeza ushindani wa kuwania namba katika kikosi cha kwanza.
Pia wale ambao, wanakaa benchi ni vyema wakaongeza jitihada ili kuongeza ushindani wa kuwania namba. Kwa kufanya hivyo wanaweza kujiongezea kipato chao.
SWALI: Kitu gani hadi sasa ambacho kinakukera katika michuano ya ligi kuu iliyomalizikia hivi karibuni?
JIBU: Nachukizwa na baadhi ya waamuzi kushindwa kutafsiri vyema sheria 17 za soka ili mshindi aweze kupatikana kwa haki.
Wapo baadhi ya waamuzi, ambao ni chanzo cha timu nyingi kufanya vibaya kutokana na tabia zao za kutaka kuzibeba timu, ambazo hazina uwezo na kusababisha zishindwe kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa. Mbali na hayo, ninachukizwa na tabia ya wachezaji kuhujumu timu kama kigezo cha kutaka maslahi au kudai haki.
Hili ni jambo baya kwa vile zipo taratibu husika, ambazo zinapaswa kufuatwa na wachezaji katika kudai haki zao na zikapatikana. Hivyo ni vyema wachezaji watekeleze majukumu yao uwanjani bila kuziathiri timu zao.
Kuna jambo lingine, ambalo limekuwa likinikera sana, lakini sina ushahidi nalo. Lakini kama kweli lipo, ni vyema wanaofanya hivyo wakaacha mara moja ili kujenga heshima ya mchezo huo.
SWALI:Una maoni gani kuhusu timu ya Taifa Stars?
JIBU: Kwa kweli naona hali inazidi kuwa ngumu hata kwa Kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen ambaye hadi sasa hana kikosi cha kwanza.
Kila kukicha utakuta anajaribu wachezaji mbalimbali ili kusaka kikosi cha kwanza kutokana na uwezo wa wachezaji kupanda na kushuka. Nina imani kwamba soka ina mambo mawili ya msingi, kujituma na kusikiliza mafunzo ya kocha ili malengo ya ushindi yaweze kutimia.
SWALI: Una maoni gani kuhusu timu za Simba na Yanga ambazo mwakani zitawakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa?
JIBU: Nawaomba viongozi wa benchi la ufundi wa timu hizo kuwa makini sana katika kipindi hiki cha usajili ili kuwapata wachezaji wenye uwezo wa kuzisaidia timu zao.
Hakuna jambo jingine kwa mchezaji kama kuweka historia ya kuwa mchezaji fulani aliweza kuchangia matokeo mazuri katika michuano ya Afrika na timu hizo ziweze kupata matokeo mazuri kwa kujiandaa na kucheza michezo mingi ya majaribio ndani na nje ya nchi.
Vilevile nawaomba wachezaji wa Yanga na Simba tuzingatie mafunzo ya walimu wetu ili tuweze kuwa katika kiwango cha hali ya juu.

No comments:

Post a Comment