'
Thursday, April 28, 2011
Bado nasaka timu Ulaya-Cannavaro
BEKI kisiki wa klabu ya Yanga, Nadir Haroub 'Canavaro' amesema bado anaendelea na mikakati ya kwenda kucheza soka ya kulipwa barani Ulaya.
Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, Cannavaro alisema hajafuta mpango wake huo kwa sababu moja ya malengo yake ni kujiendeleza zaidi kisoka.
Cannavaro ameelezea msimamo wake huo, kufuatia kuwepo na taarifa kwamba, klabu ya Azam inafanya mipango ya kumsajili kwa ajili ya msimu ujao.
Licha ya kuwepo kwa mipango hiyo, uongozi wa Yanga ulikaririwa hivi karibuni ukisema kuwa, hauna mpango wa kumuuza mchezaji huyo kwa klabu ya Azam.
"Napenda kwenda kucheza soka nje ya nchi ili kuongeza kipato na kujiandaa kwa maisha yangu ya baadaye baada ya kustaafu soka, lakini nitaendelea kuwepo Yanga hadi mpango huo utakapotimia,"alisema beki huyo.
Kwa mujibu wa Cannavaro, amekuwa akifanyakazi ya kusaka timu nje kwa kushirikiana na baadhi ya mawakala wa hapa nchini na wa nje.
Cannavaro aliwahi kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada akiwa na Nizar Khalfan mwaka juzi, lakini alikwama kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Nizar ndiye pekee aliyeweza kuvuka visiki vya majaribio katika klabu hiyo na hadi sasa ni mmoja wa wachezaji wanaotegemewa kwenye kikosi cha kwanza.
“Mipango yangu yote inafanyika kwa uwazi mkubwa, siwezi kuuficha uongozi wa Yanga. Mambo yatakapokuwa tayari, nitatoa taarifa kwa uongozi,”alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment