'
Friday, April 8, 2011
Manji arejesha logo Yanga
MFADHILI Mkuu wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji ameamua kurejesha mali mbalimbali za klabu hiyo na kuamua kutojihusisha na jambo lolote, ikiwa ni pamoja na usajili wa wachezaji wapya. Mali zilizorejeshwa na Manji kwa klabu hiyo ni pamoja na logo ya Yanga na gazeti la Yanga Imara, lililokuwa likimilikiwa na klabu hiyo. Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa, Manji amefikia uamuzi huo baada ya kuona hali si shwari ndani ya klabu hiyo. Kwa mujibu wa habari hizo, Manji amemueleza Katibu Mkuu wa muda wa klabu hiyo, Celestine Mwesingwa kwamba ameamua kufanya hivyo kwa sababu hafurahishwi na mgogoro ulipo sasa Yanga. Logo ya Yanga ilisajiliwa na uongozi wa zamani uliokuwa chini ya Iman Madega, ambapo Manji aliingia nao mkataba na kukubaliana kuilipa klabu hiyo sh. milioni 12.5 kila mwezi. Kufuatia mkataba huo, mtu yoyote aliyekuwa akitaka kutengeneza kitu chochote chenye nembo ya Yanga, alipaswa kuwasiliana na Manji ili klabu hiyo iweze kunufaika kimapato. Uamuzi huo wa Manji umewaweka kwenye wakati mgumu viongozi wa Yanga, akiwemo Mwesingwa, ambaye ameshauriwa na mfadhili huyo afunge ofisi anayoitumia ndani ya jengo la klabu hiyo. Tayari ofisi ya katibu mkuu huyo wa Yanga imeshafungwa na kuna habari kuwa, Manji amepanga kuwalipa madai yao wachezaji wote wa klabu hiyo na watendaji wengine mwishoni mwa mwezi huu. “Manji hafurahishwi na hali ilivyo sasa ndani ya Yanga, hasa mvutano uliozuka baina ya Mwenyekiti Lloyd Nchunga na makamu wake,David Mosha, ambaye alitangaza kujiuzulu,” kilisema chanzo cha habari. Mbali na kutofurahishwa na mvutano huo, chanzo hicho kilisema Manji amekerwa kuona Yanga imeshindwa kupata mafanikio katika ligi ya msimu huu na michuano ya kimataifa, ambapo ilitolewa raundi ya kwanza. Kubwaga manyanga kwa Manji kumempa hofu kubwa Nchunga kuhusu usajili wa wachezaji wapya kwa ajili ya msimu ujao wa ligi. Manji ndiye aliyekuwa akigharamia usajili wa wachezaji na kuwalipa mishahara. Kuna habari kuwa, baadhi ya wachezaji nyota wa Yanga wameweka msimamo wa kufungasha virago msimu ujao kutokana na kutokuwa na uhakika wa ajira yao kufuatia Manji kubwaga manyanga. Mbali na kufadhiliwa na Manji, Yanga pia imeingia mkataba na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambayo hulipa sehemu ndogo ya mishahara ya wachezaji. Juhudi za kumpata Manji jana zilishindikana kutokana na kila mara simu yake ya mkononi ilipopigwa, kupokewa na msaidizi wake, ambaye alidai kuwa, bosi wake huyo alikuwa kwenye kikao. Habari zaidi zimeeleza kuwa, uongozi wa klabu hiyo upo mbioni kumwangukia aliyekuwa makamu mwenyekiti Mosha ili kumshawishi arejee madarakani kwa lengo la kuokoa jahazi la usajili wa wachezaji msimu ujao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment