LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI nyota wa filamu nchini Nigeria, Ini Edo amekiri kuwa amechoka kufanya kitu kile kile katika sinema anazoigiza na kwamba ameweka msimamo wa kutofanyakazi, ambazo hazimvutii.
Ini, mzaliwa wa Jimbo la Akwa Ibom nchini Nigeria, alisema wiki hii kuwa, miongoni mwa mambo yasiyomvutia katika fani hiyo hivi sasa ni maelezo yasiyo na mvuto katika baadhi ya sinema.
Mwanadada huyo, ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa balozi wa Umoja wa Mataifa wa mazingira alisema anasikia faraja kubwa kupewa heshima hiyo kwa vile ni nafasi nzuri kwake kutoa mchango wake kwa jamii na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Alisema kutokana na wadhifa wake huo, moja ya majukumu yake makubwa ni kuwasaidia watoto wa aina hiyo ili kuwaokoa katika maisha hatarishi.
“Kama tutawapa watoto hawa nafasi sahihi, kuwaunga mkono na kuwapa moyo, lazima watabadilika,”alisema mcheza sinema huyo wa Nollywood, aliyecheza filamu lukuki.
“Hakuwaumba kuishi walivyo. Hakutaka waishi mitaani, chini ya madaraja ama kufa wakiwa na umri mdogo. Mazingira yetu ndiyo yaliyosababisha waishi hivyo.
“Wajibu wangu nikiwa balozi wa Umoja wa Mataifa ni kuwasaidia kulingana na uwezo wangu na kuwasaidia watu hawana kuondokana na maisha hayo. Naelewa haitakuwa kazi nyepesi, lakini hilo ni jukumu langu.
“Mbali na kucheza filamu na kuwafurahisha watu kupitia kwenye video, tunapaswa kujifunza kuwapa misaada na kugusa maisha yao,”alisema nyota huyo wa Nollywood.
Ini alisema hakuwahi kutumia mbinu zozote ili kutaka apewe wadhifa huo na kuongeza kuwa, alipigiwa simu kuelezwa kuhusu uteuzi huo wakati akiwa kazini.
Mwanadada huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto alisema si rahisi kwa mtu yeyote kutumia mbinu ili apate uteuzi huo na kwamba haamini iwapo wapo watu wa aina hiyo.
Ini alisema viongozi wa Umoja wa Mataifa wanatambua wazi kuwa, kwa kuwatumia wasanii wa aina yake, ni rahisi kuwafanya watu washiriki katika kazi za kusaidia jamii, hasa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.
“Uteuzi huu ulikuja moja kwa moja kutoka Umoja wa Mataifa na tulifanya mkutano na waandishi wa habari nchini Kenya. Ramsey Nouah na mwigizaji mmoja kutoka India nao pia waliteuliwa kuwa mabalozi wa umoja huo,”alisema.
Ini alikiri kuwa, tangu alipofunga ndoa mwaka jana, hajashiriki kucheza filamu nyingi kwa vile amechoka kufanya vitu vinavyofanana. Alisema baadhi ya filamu za Kinigeria hivi sasa hazina mvuto kutokana na kutokuwa na mambo mapya. “Inasikitisha kusikia watu wakizilinganisha filamu zetu na za nchi jirani. Tunaweza kufanya vizuri zaidi, hiyo ndiyo sababu iliyonifanya niamue kucheza filamu zenye kiwango cha juu pekee. Kama filamu haina kiwango, sichezi,”alisema.
“Watu wamechoka kutazama kazi zisizokuwa na mvutu, ambazo baadhi ya watu wanazitengeneza na mbaya zaidi baadhi yetu sura zetu zinaonekana,”aliongeza.
Akifafanua, Ini alisema uamuzi wake huo hauna maana kwamba hatashiriki kucheza filamu zinazotengenezwa Asaba na Enugu, bali filamu yoyote, ambayo haitakuwa na mvuto bila kujali wapi itachezwa.
“Kazi mbaya haihusiani na mazingira ya eneo litakalotumika kutengeneza filamu. Unaweza kwenda kupiga picha za sinema Marekani wakati filamu nzuri inaweza kutengenezwa Zamfara. Kama nitapata maelezo mazuri ya sinema kutoka Asaba ama Enugu, nitakwenda na kama nitapata hadithi mbaya kutoka Marekani, siwezi kwenda,”alisema.
Ini alisema wakati umefika kwa wacheza sinema nchini Nigeria kuwa na msimamo ili fani hiyo iweze kupiga hatua zaidi kimaendeleo na kusisitiza kuwa, kazi mbaya zisipewe nafasi.
Mwanadada hiyo alisema watayarishaji wengi wa sinema waliopo Asaba na Enugu ni rafiki zake na wanamwelewa kuhusu msimamo wake huo. Alisema baadhi ya wakati amekuwa akiwarejeshea pesa zao baada ya kusoma maelezo ya sinema na kutoridhishwa nayo.
“Hili si suala binafsi, ni msimamo wa kikazi kwangu. Nimeamua kucheza filamu zenye kiwango pekee. Nataka kufanyakazi zitakazonifanya nione fahari wakati wote,”alisema.
Kwa sasa, Ini anashiriki kuandaa filamu mpya ya ‘I’ll take my chances’, akishirikiana na mtayarishaji maarufu Emem Isong. Alisema wametumia fedha nyingi kuandaa filamu hiyo, ikiwa ni pamoja na wapiga picha kutoka nje ya nchi.
Ini alitamba kuwa, filamu hiyo ndiyo pekee bora aliyoshiriki kuitunga na kuicheza na amewataka mashabiki kuisubiri kwa hamu kubwa kwa sababi itakuwa ya aina yake. Alisema filamu hiyo itaingizwa sokoni kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Mwanadada huyo mwenye tabasamu la bashasha alisema anafurahia maisha yake ya ndoa kwa sababu yeye na mumewe wanaelewana vyema. Alisema kazi yake haiwezi kuyaathiri maisha hayo.
“Tunazo baadhi ya changamoto, lakini tumekuwa tukiyatatua baadhi ya matatizo yanayojitokeza na kusonga mbele na maisha. Namfurahia mtu wangu huyu na ndoa yangu,”alisema.
Ini alikanusha madai kuwa, amekuwa hana uhusiano mzuri na wacheza filamu wenzake, Oge Okoye, Uche Jombo na Mercy Johnson. Alisema hana ugomvi wowote na wasanii hao.
“Sina ugomvi na watu hawa. Mimi ni mtu wa amani. Mwaka huu sitarajii kurudi nyuma, nasonga mbele. Baadhi ya watu hawa ni rafiki zangu, wengine ni watu wangu wa karibu,”alisisitiza.
Licha ya kuolewa, Ini amekiri kuwa baadhi ya wanaume wamekuwa wakimsumbua kwa kumtaka kimapenzi, lakini alisisitiza kuwa, hawezi kuwapa nafasi kwa vile anayafurahia maisha yake ya ndoa.
“Pete ya ndoa haiwazuii wanaume kukufuatafuata, nadhani ndiyo inayowavutia zaidi. Wanadhani utakuwa tayari kufanya nao mapenzi na huwezi kuwasumbua kama wanavyofanya wanawake, ambao hawajaolewa,”alisema.
“Naifurahia ndoa yangu, sihitaji bega la mwanaume yeyote. Na nahitaji kusema hivi kwa wanawake wengine; furaha katika maisha inakuja kutoka kwa penzi la mwanaume umpendaye. Kama utaifanyiakazi ndoa yako na kumuomba Mungu, atakusaidia,”alisisitiza.
No comments:
Post a Comment