'
Thursday, April 28, 2011
Filamu za 'Inye' zapigwa marufuku
SERIKALI imepiga marufuku kuonyeshwa hadharani na kwenye vyombo vya usafiri filamu tano zilizokaguliwa na kubainika kuwa zinakiuka maadili ya kitanzania.
Filamu zilizopigwa marufuku ni Mtoto wa Mama, Inye, Inye Plus, Inye Ndembendembe na Inye Gwedegwede.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza jana ilisema kuwa, filamu ya Shoga imeruhusiwa kuonyeshwa hadharani baada ya waandaaji kuifanyia marekebisho.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kati ya Februari na Machi mwaka huu, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kupitia Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza, ilifanya ukaguzi wa filamu 45, kati ya hizo zilizoruhusiwa kuonyeshwa ni 40 na zilizozuiwa kutokana na kutozingatia maadili ya Kitanzania ni tano.
“Sababu za kukataliwa ni pamoja na filamu hizo kutokuwa na maudhui na maadili ya Kitanzania, kwa kuwa zinaonyesha vitendo vya ushoga pia zinadhalilisha wanawake, hasa wanene kwa kugeuza miondoko yao, ambayo inaamsha hisia za kingono,”ilisema taarifa hiyo. “Filamu ya Mtoto wa Mama ni ya daraja ‘R’, yaani hairuhusiwi kuonyeshwa mahali popote na wakati wowote nchini Tanzania kwani inaonyesha vijana wa kiume wanaovaa na kuishi maisha ya kike (mashoga),”iliongeza.
“Filamu za Inye, Inye Plus, Inye Ndembendembe na Inye Gwedegwede zipo katika daraja hilo hilo kwani zinahusu vichekesho vinavyozingatia sana maumbile ya miili ya wanawake na miondoko yao, ambayo inaamsha hisia za kingono,” ilisema taarifa hiyo.
Bodi hiyo ya filamu imewataka watunzi na watengenezaji wa filamu kutotengeneza filamu bila kuwa na kibali cha waziri mwenye dhamana ya masuala yanayohusu filamu na michezo ya kuigiza na kutoonyeha filamu yeyote bila kukaguliwa na kupewa daraja. Wakati huo huo, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeridhia marekebisho yaliyofanywa katika filamu ya Shoga Yangu, ambayo hapo awali ilikuwa ikiitwa Shoga.
Taarifa ya wizara hiyo ilisema jana kuwa, marekebisho hayo yaliwasilishwa Aprili 8, 2011 na filamu hiyo imepewa daraja‘A’ 18.
“Filamu hiyo sasa inafaa kuangaliwa na watu wazima kuanzia miaka 18 na kuendelea. Marekebisho yaliyoelekezwa kufanyika katika filamu hiyo yalikuwa ni pamoja na kipande cha bafuni kinachoonyesha mashoga wakiwa wanaoga, kilitakiwa kuondolewa, maneno makali yanayotamkwa kiuhalisia yalitakiwa kutafutiwa maneno mbadala pia jina la filamu (Shoga) lilitakiwa kubadilishwa kwa kuwa halikuwa linaendana na maadili ya Kitanzania,” ilisema taarifa hiyo. Wizara imemtaka mtengenezaji wa filamu hiyo kutotumia tangazo lililotumika kuitangaza filamu hiyo hapo awali kwani haliendani na maudhui yaliyomo katika filamu baada ya marekebisho.
Awali, filamu ya Shoga ilipigwa marufuku kuonyeshwa hadharani, kufuatia kuandaliwa katika mazingira yanayokiuka maadili ya Mtanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment