KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 28, 2011

Kigogo Lyon amaliza sakata la Samatta

HATIMAYE sakata la mchezaji Mbwana Samatta huenda likafikia ukingoni baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wa African Lyon, Jamal Kisongo kusema kuwa yeye ndiye aliyemhamisha mchezaji huyo kwenda Simba.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kisongo alisema haoni sababu ya uongozi wa African Lyon kumng'ang'ania mchezaji huyo wakati alihamishwa kihalali.
Kisongo alisema wakati akiwa kiongozi katika klabu hiyo, alimshauri Samatta kukubali kuhamia Simba kwa ajili ya kuendeleza kipaji chake.
Alisema alisimamia hatua kwa hatua uhamisho wa mchezaji huyo na kuhakikisha anahamia Simba huku sheria na kanuni halali zikitumika katika uhamisho huo.
Alisema Samatta alikubali na akapelekewa fomu akiwa katika kambi ya timu ya taifa ya vijana na kumalizana na Simba huku African Lyon chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Jeshi Zakaria akitia ubani kubariki kuondoka kwa mchezaji huyo.
Alisema baada ya Samatta kuondoka, African Lyon iliuzwa kwa wamiliki wa sasa wakati huo mchezaji huyo akiwa akiwa tayari amehama na kusema anashangaa kuona viongozi hao wanadai ni mchezaji wao wakati si kweli.
Alisema kutokana na hali hiyo, haoni sababu za viongozi wa sasa kuendeleza sakata hilo jambo ambalo litamchanganya mchezaji huyo na kushindwa kucheza.
Alisema kama African Lyon inataka fedha kidogo ni bora wakaongea na Simba na kumuacha mchezaji huyo akakuze kipaji chake pamoja na kwenda kujitafutia riziki yake.
Alisema hata kama Samatta ataichezea klabu hiyo, hakuna mtu yeyote atakayekuwa na mamlaka naye zaidi ya wakala wake, familia yake na klabu ya TP Mazembe.
Sakata la Samatta lilianza kuchukua kasi baada ya uongozi wa klabu ya Simba kutangaza kumuuza kwa klabu ya TP Mazembe kwa zaidi ya sh. milioni 150.
Baada ya hapo, wamiliki wa sasa wa klabu ya African Lyon waliibuka na kudai fedha za mauzo ya mchezaji huyo wanatakiwa wapewe wao kwa kuwa ni mchezaji wao halali.
Hata hivyo, sakata hilo bado halijapatiwa ufumbuzi hadi sasa kwa kuwa kila kukicha kumekuwa kukiibuka madai na malumbano tofauti.

No comments:

Post a Comment