UONGOZI wa klabu ya Simba umeshtukia mpango wa timu ya Azam FC kutaka kuwanasa baadhi ya nyota wake, akiwemo Emmanuel Okwi, kufuatia hivi karibuni kumnasa beki Joseph Owino.
Habari zilizothibitishwa na kiongozi mmoja wa juu wa Simba zimeeleza kuwa, wamesikitishwa na kitendo cha viongozi wa Azam kuteta na baadhi ya wachezaji wao, ambao bado wana mikataba.
Alisema kitendo kinachofanywa na viongozi wa Azam ni kibaya na wao wana uwezo wa kukifanya, lakini wanaheshimu sheria za usajili zinavyosema.
Kiongozi huyo, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini alisema, wameshapata taarifa kwamba Azam imeshamsajili kiungo wao, Abdulhalim Humud bila kuzungumza na uongozi wa Simba.
Simba imekumbwa na hofu kuhusu Okwi baada ya kuwepo taarifa kwamba anatakiwa kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa kwa klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Simba, taarifa hizo ni za uzushi kwa vile wamebaini hizo ni mbinu zinazofanywa na wapinzani wao kutaka kumsajili mshambuliaji huyo kutoka Uganda. Okwi pia anawindwa kwa udi na uvumba na Yanga.
Hivi karibuni, Azam ilitangaza rasmi kumsajili kipa wa zamani wa Yanga, Obren Cirkovic. Pia kulikuwa na habari kwamba, klabu hiyo inataka kuwasajili kipa Juma Kaseja na mshambuliaji Mussa Hassan ‘Mgosi’ wa Simba.
Hata hivyo, mipango ya Azam kuwasajili Kaseja na Mgosi ilikwama baada ya kuwepo na taarifa kwamba, bado wana mikataba na Simba. Lakini kuna habari kuwa, huenda wachezaji hao wakatemwa na Simba msimu ujao.
"Haiwezekani timu ikutane na mchezaji bila ya kufanya mazungumzo na klabu yake husika ili iweze kupata ridhaa ya kufanya hivyo,kwa kweli hili ni jambo baya,"alionya kiongozi huyo wa Simba.
Aliongeza kuwa, wakati klabu yake ilipokuwa ikifanya mipango ya kumsajili Salum Machaku kutoka Mtibwa Sugar, iliwasiliana kwanza na viongozi wake na kupata ruhusa.
"Hawa Azam ni watu wa ajabu, sisi tunaweza fujo, ambazo wanazifanya,lakini tunaheshimu sheria, vinginevyo tuna uwezo wa kusajili wachezaji wote tunaowahitaji kutoka timu yao,” alisema.
Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti hivi karibuni kuwa, Azam imefanikiwa kumnasa Owino, ambaye alikuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Mchezaji huyo aliondoka Simba baada ya kuumia katika michuano ya kombe la Chalenji na kumfanya afanyiwe upasuaji wa goti nchini India. Kuna habari kuwa, matibabu hayo yaligharamiwa na uongozi wa Azam.
Mwenyekiti wa Azam, Said Mohamed alipotakiwa kuzungumzia jambo hilo, alisema wana kikao kuhusu mambo mbalimbali, ikiwemo usajili wa wachezaji na kumtaka mwandishi wa habari hizi ampigie simu baadae.
Wakati hayo yakiendelea, Simba inatarajiwa kukamilisha mpango wa kumnasa beki Patrick Mafisango, ambaye alijiunga na Azam mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea APR ya Rwanda.
Mafisango, ambaye alizaliwa Machi 7,1987 nchini Rwanda, imeelezwa kwamba anatarajiwa kuziba pengo la Owino. Pia kuna habari kuwa, Simba inataka kumrejesha kiungo wake, Ramadhani Chombo, aliyejiunga na Azam msimu uliopita.
No comments:
Post a Comment