'
Friday, April 8, 2011
Bongo Fleva yamnogesha Dully Sykes
SIKU chache baada ya kudondosha ngoma mpya inayokwenda kwa jina la ‘Bongo Fleva’, msanii Dully Sykes ameamua kushusha kigongo kingine cha ‘Remix’ ya wimbo huo. Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Dully alisema ameamua kufanya hivyo kutokana na wimbo huo kupokelewa vizuri na mashabiki wake. “Nashukuru kuona kwamba mashabiki wangu wameupokea vizuri wimbo huu ndio sababu nimepata mzuka wa kufanya remix yake,”alisema msanii huyo machachari. Amewataja wasanii alioshirikiana nao kurekodi ‘remix’ hiyo kuwa ni pamoja na Profesa Jay, Lady JayDee na Mwana Falsafa. Alisema ameamua kuwapa shavu wasanii hao katika kibao hicho kwa sababu ya uzito wao na heshima yao katika muziki wa kizazi kipya. “Nimewapa heshima hiyo wasanii hawa kwa sababu wamekaa kwenye game kwa muda mrefu sana,”alisema Dully, ambaye kabla ya kibao hicho, alitamba kwa wimbo wake wa ‘Shekide’. Amewataka mashabiki wake kukaa mkao wa kula kukisubiri kibao hicho kwa sababu kitakuwa moto wa kuotea mbali kuliko kile cha awali. Dully, ambaye ni mtoto wa mkongwe wa muziki nchini, Ebby Sykes alianza kupata umaarufu mwanzoni mwa miaka ya 2000 alipoibuka na albamu yake ya kwanza ya ‘Historia ya Kweli’. Kabla ya albamu hiyo, msanii hiyo alitamba kwa vibao vyake vya ‘Julieta’, ‘Salome’, ‘Leah’. Mwaka 2003 aliibuka na albamu ya ‘Handsome’ kabla ya kushusha albamu ya ‘Hunifahamu’ mwaka 2005. Mwaka 2004, Dully alishinda tuzo ya albamu bora ya hip hop kupitia albamu ya ‘Handsome’ na kibao chake cha ‘Dhahabu’ kilishinda tuzo ya wimbo bora wa kushirikisha wasanii wengine. Aliimba wimbo huo kwa kuwashirikisha Joslin na Mr. Blue. Msanii huyo pia aling’ara mwaka 2008 baada ya kibao chake cha ‘Baby Candy’ kushinda tuzo ya wimbo bora wa reggae. Baadaye aling’ara kwa vibao vya ‘Nyambizi’ na ‘Kuche Kuche’.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment