Leila Rashid
Isha Mashauzi
WAIMBAJI tegemeo wa kundi la muziki wa taarab la Jahazi, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’ na Leila Rashid wanadaiwa kusimamishwa kazi katika kundi hilo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kundi hilo zimeeleza kuwa, waimbaji hao wawili wamesimasishwa kazi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kujiona mastaa.
Chanzo hicho kilisema, kwa muda mrefu Isha na Leila wamekuwa wakileta mapozi wakati wa maonyesho ya kundi hilo, hali iliyoufanya uongozi uamue kuwasimamisha kwa muda.
"Ulifika wakati waimbaji hawa wakawa wanaonekana mzigo katika kundi ndio sababu wamesimamishwa kwa sababu wapo waimbaji wengi wenye vipaji,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, uamuzi wa kuwasimamisha Isha na Leila umelenga kutoa funzo kwa wasanii wengine wa kundi hilo wenye tabia kama hizo.
Chanzo hicho kilizidi kupasha kuwa, mara nyingi Isha alikuwa akichelewa kufika mazoezini na kwenye maonyesho na kila alipoonywa, alionyesha dharau.
Hata katika uzinduzi wa albamu ya saba ya kundi hilo uliofanyika Jumapili iliyopita katika ukumbi wa Travertine, Magomeni, Dar es Salaam, waimbaji hao wawili hawakuonekana ukumbini.
Kukosekana kwa waimbaji hao mahiri kulizusha hisia tofauti miongoni mwa mashabiki waliojitokeza katika uzinduzi huo, ambapo wengi walipongeza uamuzi uliofanywa wa kuwasimamisha kazi.
"Ni bora walivyosimamishwa, walikuwa wanalifanya kundi hili kama la kwao,” alisema mmoja wa mashabiki waliohudhuria onyesho hilo.
“Isha mwenyewe alikuwa akifika kwenye maonyesho kwa muda anaotaka, hii ni dharau kubwa kwa uongozi," aliongeza shabiki mwingine.
Uzinduzi wa albamu hiyo ulifana vilivyo kutokana na waimbaji chipukizi waliojiunga na kundi hilo hivi karibuni kuonyesha umahiri wa hali ya juu. Waimbaji hao ni Mohammed Chipolopolo na Fatuma Kasim.
No comments:
Post a Comment