KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, April 8, 2011

Vijana Stars yaikamia Cameroon

TIMU ya soka ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 23, Vijana Stars imetamba kuwa, itatoa kipigo kwa Cameroon katika mechi yao ya marudiano. Vijana Stars na Cameroon zitarudiana kesho katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Olimpiki za mwaka 2013, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, mshambuliaji Mbwana Samatta alisema wamepania kuitoa nishai Cameroon na kutoa onyo kwa timu zingine zinazoshiriki michuano hiyo. Samatta alisema wamefanya mazoezi ya kutosha kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi hiyo na kuongeza kuwa, wana uhakika mkubwa wa kuibuka na ushindi. "Hatutishiki na Cameroon kwa sababu ni timu ya kawaida tu. Uwezo wa kuishinda na kusonga mbele tunao kwa sababu wachezaji wote wana ari kubwa,"alisema. Katika mechi ya awali, iliyochezwa wiki mbili zilizopita mjini Yaounde, Cameroon iliichapa Vijana Stars mabao 2-1. Ili isonge mbele, Vijana Stars inahitaji ushindi wa bao 1-0. Wakati huo huo, mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), Said Hamad El-Maamry anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika pambano kati ya Vijana Stars na Cameroon. Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, El-Maamry amethibitisha kuhudhuria pambano hilo.

No comments:

Post a Comment