KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 24, 2011

Sam Timbe awazulia balaa mastaa Yanga

KOCHA Mkuu wa Yanga, Sam Timbe amezua hofu miongoni mwa wachezaji mastaa wa timu hiyo baada ya kueleza kwamba atawatimua wale wote walio wazembe na watovu wa nidhamu.
Kufuatia kauli na msimamo huo wa Timbe, baadhi ya wachezaji wanaojiona kuwa ni nyota katika klabu hiyo wameanza kupatwa na mchecheto na kusaka timu za kuchezea msimu ujao.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani wiki hii umebaini kuwa, uamuzi huo wa Timbe umekuja baada ya kubaini kuwa, baadhi ya wachezaji hawazingatiaa ratiba ya mazoezi na kujiona ni bora kuliko wenzao.
Msimamo huo wa Timbe umewafanya wachezaji kama vile Ernest Boakye kuonekana mara kwa mara kwenye ofisi za Azam na African Lyon kwa lengo la kusaka usajili msimu ujao.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Burudani, Boakye ni mmoja wa wachezaji, ambao wamekuwa wakionyesha vitendo vya utovu wa nidhamu na hivyo kumtibua Timbe.
Hivi karibuni, Boakye alidaiwa kugoma kufanya mazoezi wakati Yanga ilipokuwa ikijiandaa kumenyana na Azam mjini Tanga na kusababisha aondolewe kambini.
Boakye pia alidaiwa kutaka kuihujumu Yanga ilipokuwa ikijiandaa kumenyana na Simba katika mechi ya ligi kuu, hali iliyosababisha asichezeshwe.
Mchezaji mwingine, ambaye amedaiwa kuanza kusuka mipango ya kuihama na timu hiyo ni Yaw Berko. Kipa huyo anadaiwa kutaka kujiunga na mojawapo kati ya timu za Simba na Azam.
Wachezaji wengine wanaodaiwa kufanya mipango hiyo ni viungo Athuman Idd 'Chuji' na Nurdin Bakari na beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Mikataba ya wachezaji hao inatarajiwa kumalizika msimu ujao.

No comments:

Post a Comment