KIONGOZI wa bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, Muhidin Gurumo amelazwa tena kwenye Hopitali ya Taifa ya Muhimbili mjini Dar es Salaam baada ya hali yake kuwa mbaya. Gurumo alifikishwa kwenye hospitali hiyo jana saa moja asubuhi akiwa mahututi na kuna habari kuwa, alilazwa kwa muda kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Meneja wa bendi hiyo, Saidi Kibiriti alithibitisha jana kulazwa kwa mwanamuziki huyo kwenye hospitali hiyo, lakini hakuwa tayari kuzungumzia afya yake kiundani. “Ni kweli Mzee Gurumo amelazwa tena hapa Muhimbili na mimi ndio kwanza nafika hapa, sijapata nafasi ya kumuona, hivyo siwezi kujua nini kinamsumbua,”alisema. Kibiriti alisema alipata taarifa za kupelekwa kwa Gurumo kwenye hospitali hiyo kutoka kwa ndugu zake wa karibu, lakini hawakumweleza kilichomsibu. Hii ni mara ya pili kwa Gurumo kulazwa hospitali ya Muhimbili. Mara ya kwanza ilikuwa Februari mwaka huu, alipokuwa akisumbuliwa na homa ya kwenye mapafu. Licha ya kuruhusiwa kutoka hospitali, Gurumo alikuwa akikabiliwa na tatizo la kutembea, ambapo alikuwa akisaidiwa kufanya hivyo na mkewe. Mwanamuziki huyo mkongwe alikuwepo kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee mjini Dar es Salaam wakati Msondo Ngoma ilipofanya onyesho la pamoja na Mlimani Park Orchestra wiki mbili zilizopita.
No comments:
Post a Comment