KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, March 25, 2011

Simba, TP Mazembe kurudiana mchana


MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amesema mchezo kati yao na TP Mazembe utafanyika saa tisa mchana ili kuwachosha wapinzani wao.
Akizungumza na Burudani mwanzoni mwa wiki hii mjini Dar es Salaam, Rage alisema wameandaa mikakati kabambe ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kusonga mbele.
Simba na TP Mazembe zinatarajiwa kurudiana wiki mbili zijazo katika mechi ya raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika. Katika mechi ya awali iliyochezwa wiki iliyopita mjini Lubumbashi, Simba ilichapwa mabao 3-1.
Ili iweze kusonga mbele katika michuano hiyo, Simba italazimika kuishinda TP Mazembe mabao 2-0 na kutowaruhusu wapinzani wao kupata bao la ugenini.
“Tuna hakika tukiwachezesha TP Mazembe katika muda huo, watachoka haraka na hiyo itatupa nafasi ya kushinda mechi hiyo kirahisi,”alisema Rage.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema hali ya hewa ya mji wa Lubumbashi ni ya baridi kali na ndio sababu waliamua kwenda kuweka kambi Arusha kujiandaa na pambano la awali.
Mbali na kutumia mbinu hiyo, Rage alisema wamepanga kuiandaa timu yao kikamilifu ili waweze kushinda mechi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwaongezea hamasa wachezaji.
“Tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi katika mechi hiyo ili kuwaongezea hamasa wachezaji kwa sababu uwezo wa kushinda ni mkubwa,”alisema.
Rage alisema Simba inatarajiwa kuanza kambi kati ya leo na kesho kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo. Jana, mabingwa hao wa Tanzania Bara walitarajiwa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Vijana Stars.

No comments:

Post a Comment