KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, March 25, 2011

DAISY MUSHUMBUSI, Mrembo wa Utalii mwenye vipaji lukuki


KWA umri na umbo, Daisy Mushumbuzi anaonekana kuwa mdogo. Urefu wake hauzidi futi tano. Pia ni mwembamba na rangi yake ni nyeusi, ile ya asilimia. Ni mwenyeji wa mkoa wa Bukoba.
Daisy (24) ndiye aliyeibuka kuwa mshindi wa taji la kipaji katika shindano la Miss Utalii 2011 lililofanyika mwanzoni mwa mwezi huu kwenye hoteli ya Kiromo iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani.
Isingekuwa kigezo cha urefu, pengine Daisy ndiye angeibuka mshindi wa taji hilo kwani ana uelewa wa hali ya juu kuhusu masuala mbalimbali duniani. Pia ana uelewa mkubwa wa masuala ya utalii kwa vile ni fani aliyoisomea.
Hata Mkurugenzi wa Kamati ya Miss Utalii, Gideon Chipungahelo anakiri juu ya ukweli huo kwa kusema, binti huyo ana akili za kipekee na kwamba kilichomwangusha ni umbo lake.
Daisy ana shahada ya usimamizi wa utalii aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Moi kilichopo mjini Nairobi, Kenya. Ni mtoto wa nne katika familia ya watoto watano wa Mzee Mushumbuzi.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Daisy alisema alishawishika kushiriki kwenye mashindano hayo kwa vile fani hiyo ipo kwenye damu yake. Alisema alikuwa akipenda mambo ya utamaduni, hasa uchezaji ngoma tangu akiwa shule ya msingi.
“Binafsi nimesomea fani ya utalii, ni taaluma yangu na nimekuwa nikiipenda tangu nikiwa mdogo ndio sababu nilianza kushiriki kwenye shindano hili kuanzia ngazi ya mkoa wa Kagera,”alisema.
Daisy alisema amejifunza mengi kutokana na ushiriki wake katika mashindano hayo, ikiwa ni pamoja na kuufahamu vyema utalii wa ndani na kutembelea vivutio vinane vya utalii kati ya 16 vilivyopo nchini.
Mrembo huyo mwenye haiba ya kuvutia pia alisema ushiriki wake kwenye mashindano hayo umemwezesha kujifunza jinsi lugha ya Kiswahili ilivyoweza kuwaunganisha pamoja watanzania licha ya kuwepo na makabila zaidi ya 120.
Alisema amepanga kutumia taji lake la mrembo mwenye kipaji kuutangaza vyema utalii wa ndani ya nchi na pia kuwashawishi vijana wenzake wa kike kujitosa kwenye fani ya urembo na kuondokana na dhana kwamba ni ya kihuni.
Mrembo huyo anayependa kuogelea, kuimba na kucheza ngoma za kiasili alisema, ana hakika binadamu yoyote mwenye kipaji akikitumia vyema, ana uwezo mkubwa wa kufanikiwa katika maisha yake hivyo amewataka vijana wenzake wenye vipaji kujitokeza hadharani.
Aliyataja baadhi ya malengo yake ya baadaye kuwa ni pamoja na kuanzisha kikundi cha utamaduni na kuwafundisha vijana wenzake kucheza ngoma.
“Nitafanya mipango ili nishirikiane na BASATA kuimarisha sekta ya utamaduni kwa kuzifanya ngoma za na nyimbo za asili ziwe miradi tegemezi kwa kurekodiwa kwenye CD na kanda za video,”alisema.
Alisema pia kuwa, amepania kuendeleza kipaji chake cha ubunifu wa mavazi ili aweze kuwa mjasiliamali na kujiingizia kipato. Mbali na kubuni mavazi, ana uwezo mkubwa wa kutengeneza heleni za kiasili.
“Mungu akipenda nimepanga kuanzia kampuni ya utalii na nitaitumia kuendeleza sekta hii nchini. Pia nitashirikiana vyema na waandishi wa habari katika kuutangaza utalii wa ndani,”alisema.
Akimzungumzia mshindi wa shindano la mwaka huu la Miss Utalii, Adelqueen Njozi, mrembo huyo alisema alistahili kuvikwa taji hilo kutokana na kuwa na vigezo vyote vinavyotakiwa.
“Kwa kweli mshindi wa taji hilo ana sifa zote zinazotakiwa hivyo alistahili. Ana heshima, muelewa na ana uwezo mkubwa wa kuishawishi jamii,”alisema Daisy.
Aliongeza kuwa, ana hakika Adelqueen ana uwezo mkubwa wa kufanya vizuri katika shindano la dunia la Miss Utalii, linalotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Ametoa mwito kwa wanawake wenye vipaji kujiamini na kujitokeza hadharani ili waweze kuvitumia kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao.

No comments:

Post a Comment