NEW YORK, Marekani
MCHEZA tennis nyota duniani, Serena Williams huenda akashindwa kuonekana uwanjani kwa mwaka mmoja baada ya kubainika kuwa anasumbuliwa na magonjwa mawili makubwa.
Wakala wa mchezaji huyo alithibitisha juzi mjini hapa kuwa, uchunguzi wa madaktari umeonyesha kuwa, Serena anasumbuliwa na matatizo ya kuganda damu kwenye mapafu na mishipa kuvuja damu kwa ndani.
Kwa mujibu wa madaktari, Serena alibainika kusumbuliwa na magonjwa hayo baada ya kufanyiwa operesheni wiki iliyopita na kuongeza kuwa, atalazimika kupatiwa matibabu ya muda mrefu.
Bingwa huyo mara 13 wa dunia wa mchezo wa tennis kwa wanawake, hajawahi kushiriki kwenye mashindano yoyote tangu Julai mwaka jana alipoumia mguu baada ya michuano ya Wimbledon.
“Hali ni mbaya, inatisha na kukatisha tama,”alisema Serena katika taarifa aliyoitoa juzi kupitia wakala wake.
“Naendelea vizuri. Nipo nyumbani kwa sasa na ninahudumiwa na madaktari ili kuhakikisha kila kitu kinakuwa salama. Naelewa nitakuwa salama, lakini naomba Mungu na natumaini matatizo haya yatamalizika haraka,”aliongeza.
“Kwa sasa siwezi kuahidi ni lini nitarejea uwanjani, lakini natumaini itakuwa mapema wakati wa majira ya joto. Lengo langu ni kuhakikisha nakuwa salama,”alisema.
Awali, gazeti la People lilimkariri msemaji wa mcheza tennis huyo, Nicole Chabot akisema kuwa, Serena alipatiwa matibabu ya dharula Jumatatu iliyopita baada ya hali yake kuwa mbaya.
Serena alipatiwa matibabu katika hospitali moja ya mjini Los Angeles na baadaye kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Mama wa mcheza tennis huyo, Oracene Price alisema anamshukuru Mungu kwamba hali ya binti yake huyo inaendelea vizuri.
No comments:
Post a Comment