'
Thursday, March 10, 2011
Semsekwa: Nilitimuliwa Extra Bongo kimizengwe
MWIMBAJI na rapa machachari wa bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta International, Greyson Semsekwa amedai kuwa, alitimuliwa katika bendi ya Extra Bongo Next Level kimizengwe na bila kujua tatizo lake.
Akihojiwa katika kipindi cha televisheni cha Nyumbani ni Nyumbani cha TBC 1 mwishoni mwa wiki iliyopita, Semsekwa alisema kiongozi wa Extra Bongo, Ally Choki alifikia uamuzi wa kumtimua bila kumueleza kosa lake.
“Kusema kweli Choki hakuwahi kuniita kunieleza kosa langu, nilisoma habari hizo kupitia kwenye vyombo vya habari,”alisema mwanamuziki huyo.
Semsekwa alisema katika bendi ya Extra Bongo, maamuzi yote yanafanywa na mtu mmoja (Choki) na kwamba hakuna uongozi wa pamoja.
“Mfukuze mtu kwa sababu maalumu, sio unalipuka tu. Huku ni kuvunjiana heshima,”alisema rapa huyo, ambaye alijizolea sifa kwa rapu yake inayosema ‘kichaa kapewa rungu’.
“Kabla ya kufikia uamuzi wa kumfukuza mtu kazi, unatakiwa umwite na kumweleza kosa lake na ikiwezekana unamwandikia barua na kama kuna madai yake unamlipa,”alisema.
“Yeye (Choki) baada ya kutoa taarifa hizo kwenye vyombo vya habari, akawa ananikimbia, simu anazima, kwa nini? Kiongozi wa bendi unakuwa mwoga?”aliongeza.
Semsekwa ametoa shutuma hizo kwa Choki siku chache baada ya Extra Bongo kuwatimua wanamuziki wake kadhaa na kuajiri wengine wapya saba.
Wanamuziki wapya waliochukuliwa na Extra Bongo ni pamoja na Rogert Hegga ‘Caterpilar’, Saulo John ‘Ferguson’, George Kanuti, Oseah, Isaack Buriani ‘Super Danger’, Otilia Boniface ‘Kandoro’ na Hassan Mussa ‘Super Nyamwela’
Akiwatambulisha wanamuziki hao kwa waandishi wa habari, Choki alijigamba kuwa, amepania kuifanya bendi yake iwe tishio kimuziki nchini.
Semsekwa alisema hana kinyongo na TOT na kwamba yote yaliyotokea kwake yamekwisha kwa vile ameshajipanga upya katika bendi ya Twanga Pepeta.
Alisema ameamua kujiunga na Twanga Pepeta kwamba sababu ni bendi kongwe na yenye mafanikio makubwa na pia ndiyo iliyomtambulisha kimuziki.
“Niliwahi kuimbia Twanga Pepeta kabla ya kwenda Extra Bongo. Hiki ni chuo cha mafunzo. Hata hao wanaoidharau, walipata sifa na umaarufu walipokuwa Twanga Pepeta, “ alisema.
“Nashangaa, mtu amejifunzia maisha hapa, halafu anapotoka anapadharau na kupakashifu. Huko ni kupotoka,”alisema.
Semsekwa alisema aliamua kwenda Twanga Pepeta yeye mwenyewe baada ya kupata taarifa za kutimuliwa kwake Extra Bongo na kusisitiza kuwa, hajapoteza kitu.
“Nitaibuka na mambo mapya na mazito. Nataka kule nilikitoka wajue kwamba wamepoteza chombo chenye thamani kubwa,”alisema.
“Ukiondoa Msondo Ngoma na Sikinde, hakuna tena bendi nyingine bora hapa nchini kama Twanga Pepeta. Hizi zingine ni sawa na raba za kichina. Ukitaja bendi tano bora nchini, huwezi kuikosa Twanga Pepeta. Nami niliamua nije kwenye bendi bora,”alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment